SUAMEDIA

Watanzania watakiwa kujitolea kuokoa maisha kwa kuchangia damu kwa wahitaji.

 Na; Hadija Zahoro, Morogoro.

Wananchi  wametakiwa kujenga dhana ya  utayari wa kuchangia damu kwa hiari pale wanapotakiwa kufanya hivyo na wataalamu wa afya ili kusaidia kuokoa maisha kwakuwa ni tendo la hiari lisilo na malipo.

Dkt.Erhard Kapilima katikati akizungumza kwenye kipindi cha Kapu la leo,kushto kwake ni Moses Kombo Mratibu wa damu salama Manispaa ya Morogoro na kulia kwake ni bwana Hamza Omari ambaye ni mtaalamu wa maabara hospitali za SUA. 

Wito huo umetolewa na Daktari wa magonjwa ya binadamu wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dkt.Erhard Kapilima wakati akizungumzia umuhimu wa wiki ya maadhimisho ya siku ya wachangia damu duniani katika kipindi cha Kapu la Leo kinachoruka SUAFM Redio.

Dkt. Kapilima amewaomba wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuchangia  damu  kadri wawezavyo lengo kuu likiwa  ni kuokoa maisha ya binadamu kwasababu damu ni zawadi kutoka kwa Mungu hivyo, kama mtu ana uwezo wa kutoa damu atoe kwani uhitaji wa damu ni mkubwa kuliko zinazopatikana.

‘‘Kijiografia Morogoro tupo katika barabara kuu inayogawanya njia kwenda mikoa mbalimbali ya jirani kutoka Dar es salaam, kwa maana hiyo kunakuwa na ajali za mara kwa mara zinazohusisha majeraha yanayopelekea kupoteza damu nyingi kwahiyo wanakuwa na mahitaji ya damu hivyo, kwa hospitali zetu za Morogoro ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro uchangiaji wa damu ni endelevu’’ anasema Dkt. Kapilima.

Kwa upande wake Moses Kombo, Mratibu wa Damu salama wa Manispaa ya Morogoro, amesema licha ya kutoa elimu ya kutosha bado uelewa unaenda taratibu hivyo, amewasihi wananchi kuzidi kujitolea  uchangiaji wa damu  ili kuokoa maisha ya wengine.

Ameeleza kuwa zoezi hilo  linahitaji watu wenye umri wa miaka kuanzia 18 hadi 60, uzito usiopungua kilo 50  na asiwe na magonjwa ya kudumu ikiwemo kisukari na presha na kwa upande wa wanawake mama mjamzito pamoja na anayenyonyesha.

Naye, Mtaalamu wa Maabara SUA, Hamza Omari ameeleza kuwa wao kama Hospitali ya SUA, wanashirikiana na Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kupitia matukio mbalimbali ikiwemo wiki ya kumbukizi ya sokoine na mabonanza ili kuhamasisha zoezi la uchangiaji damu na kiasi kinachopatikana huwa wanagawa katika hospitali nyingine kama vile Hospitali ya Mzinga pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Kilele cha  Maadhimisho ya Siku ya wachangia damu duniani mwaka huu,kitafa imefanyika Itega mkoani Dodoma tarehe 14  Juni  na kauli mbiu yake ni  ‘‘Changia damu, changia mazao ya damu, changia mara kwa mara, okoa maisha, huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.

Post a Comment

0 Comments