Na; Gerald Lwomile -
Kilombero
Wakati Tanzania ikiwa katika
mkakati wa kuhakikisha inajitosheleza kwa sukari nchini ifikapo mwaka 2025 na
kupunguza uagizaji wa sukari nchini ambao hugharimu zaidi ya shilingi
bilioni 161 kwa mwaka wadau wa Sukari katika Bonde la Mto Kilombero
wamekutana ili kupitia mpango kazi walioweka kuhakikisha wanawasaidia wakulima
wa miwa kuzalisha kwa tija.
Meneja wa SAGCOT Kongani ya Kilombero Bw. John Banga aliyesimama akizungumza na wadau wa Sukari (Picha zote na Gerald Lwomile) |
Miongoni mwa wadau hao ni
Kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambacho kimekusudia kuhakikisha kinapanua
kiwanda hicho kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 565 ambapo ujenzi huo
ulianza tangu Juni 2022.
Akizungumza katika kikao cha
wadau hao Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Kiwanda cha Sukari Kilombero Bw. Pierre
Redinger amesema katika kuhakikisha uzalishaji wa miwa unafanyika kwa tija
wanawaelimisha wakulima kuona kuwa wao si wafanyabiashara wa miwa tu ila ni
wakulima wafanyabiashara ambao wameingia ubia na kiwanda hicho.
Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Kiwanda cha Sukari Kilombero Bw. Pierre Redinger akizungumza katika kikao hicho |
Amesema kiwanda kimekuwa na kusudi
la kimkakati la kilimo na uzalishaji wa miwa wa ushindani na wa gharama nafuu,
salama na endelevu ili kiwanda kiwe na uwezo wa kusaga na kutumia fursa za
ukuaji wa soko la ndani hivyo kuwezesha mapato ya wakulima kutoka shilingi
bilioni 75 na kufikia shilingi bilioni 165 kwa mwaka.
“ Tuna mpamgo wa kuleta
teknolojia bora za kilimo cha miwa ambapo tutatumia zaidi ya shilingi bilioni
565 na ujenzi huu umeanza Juni 2022 na unatarajiwa kukamilika Julai 2024”,
amesema Pierre.
Akizungumza katika kikao
hicho Meneja
wa SAGCOT Kongani ya Kilombero Bw. John Banga
amesema Jukwaa hilo liliandaliwa na ofisi ya SAGCOT mwaka 2022 ili kuhakikisha
kunakuwa na ustawi katika uzalishaji wa miwa na kushirikisha Kiwanda cha Sukari,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Wizara ya Kilimo na Wakulima limeanza kutoa
matokeo chanya kwani wakulima wamefikia malengo makubwa tofauti na awali.
Meneja wa SAGCOT Kongani ya Kilombero Bw. John Banga akisisitiza jambo katika kikao hicho |
“ Kwa mfano kutoka kwenye
kilimo holela cha kulima kilimo cha miwa na kuingia kwenye mfumo rasmi ambao
unaitwa kulima kwa mpango wa kanda yaani ‘Zone’ ambao umeleta mafanikio makubwa
ambapo pia umesimamiwa na ofisi ya Mrajis wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro kwa
kushirikiana na SAGCOT na kampuni ya Sukari ya Kilombero” amesema Banga,
Amesema baada ya kuja
wawekezaji kwenye miaka ya 2000 tani moja ya miwa ilitoka kwenye bei kandamizi
ya sh. elfu 20 kwa tani moja hadi kufikia sh. elfu 65 ambapo hivi sasa tani
imefikia sh. elfu 90 jambo ambalo limehamasisha kilimo cha miwa.
Amesema mabadiliko ya
uanzishwaji wa Ushirika kutoka ule wa Chama cha Wakulima wa Miwa katika bonde
hilo umekuwa na manufaa makubwa kwani sheria iliyoanzishwa ya kuwalazimisha
wakulima wa miwa kuwa wanaushirika imetatua mizozo mingi ikiwa ni pamoja na
kuwepo kwa mpagilio mzuri wa uvunaji hata kama baadhi ya miwa itabaki shambani
kwa mwaka au zaidi.
Picha chini ni wadau wa Sukari katika Bonde la Mto Kilombero
0 Comments