SUAMEDIA

Miti zaidi ya elfu 7 kupandwa kijiji cha Chiwachiwa wilayani Kilombero

Na; Farida Mkongwe - Mlimba

Mkuu wa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro Bw. Dunstan Kyoba ameagiza kupandwa zaidi ya miche elfu 7 ya miti rafiki wa mazingira katika Kijiji cha Chiwachiwa Kata ya Mbingu Halmashauri ya Mlimba ambacho kina mito miwili muhimu ambayo ina mchango katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro Bw. Dunstan Kyoba akiwa ameshika mche wa mti tayari kwa kupanda katika kijiji cha Chiwachiwa 

Akizumgumza na wananchi katika kijiji hicho katika Siku ya Uhifadhi wa Mazingira Duniani Bw. Kyomo amesema wilaya hiyo imeamua kufanya maadhimisho hayo katika kijiji hicho ili kuendelea kuhifadhi uoto wa asili katika eneo hilo.

Amesema uwepo wa mto Lwipa na mto Chiwachiwa ambayo inapeleka maji katika mto Kilombero kunahitaji hatua za makusudi kuhakikisha inalindwa kwani mito hiyo inachangia maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linatarajia kuanza kuzalisha umeme hivi karibuni.

Mkuu huyo wa wilaya ameonya dhidi ya ukataji miti usiofuata taratibu kwa kuwa ni kosa kukata miti bila kibali cha Mkuu wa Wilaya hata kama mti huo uko kwenye makazi ya mtu kwani sheria inaelekeza kufuata utaratibu.

Awali kabla ya Mkuu huyo kuongea na wananchi Meneja wa Kongani na Ubia, Kongani ya Kilombero kutoka Taasisi ya SAGCOT Bw. John Nakei amesema haiwezekani kuwa na maisha katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kama hakuna mazingira yenye usalama na yenye afya nzuri yanayotokana na utunzaji wa mazingira.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro Bw. Dunstan Kyoba kulia akiwa na Meneja wa Kongani na Ubia, Kongani ya Kilombero katika zoezi la upandaji miti 

Amesema katika utekelezaji wa utunzaji wa mazingira wamekuwa wakishirikiana na taasisi na mashirika mbalimbali kwani wao wanao wajibu kuhakikisha wilaya ya  Kilombero inaendelea kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula nchini.

Wakizungumza katika siku hiyo ya Mazingira Duniani Bw. Abdallah Ngandu mkazi wa Kijiji cha Chiwachiwa amesema wamefuruhishwa na zoezi la upandaji miti lililofanyika katika Kijiji hicho kwani litaendelea kuhakikisha kunakuwa na hali ya hewa nzuri na kuendelea kutunza uoto wa asili katika eneo hilo.

Naye Sophia Kichumi amesema changamoto waliyopewa na Mkuu wa Wilaya ni kuhakikisha wanayatunza mazingira yao ambayo kwa kweli ni ya asili tofauti na maeneo mengine kwani uoto wa asili katika eneo lao bado umetawala kwa kiasi kikubwa.

Kauli Mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Mazingira Duniani ni "Pinga uchafuzi wa Mazingira unaotokana na taka za Plasitiki", hata hivyo wilaya ya Kilombero pamoja na kauli mbiu ya Dunia na Taifa imeongeza Kauli Mbiu yake isemayo  "Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa".

Maadhimisho hayo pia yameshirikisha wadau wengine wa Mazingira kama EWF, ISO, DEFOREST AFRICA, SAGGOT, WWF na wadau mbalimbali.








Post a Comment

0 Comments