Na: Calvin Gwabara - Arusha
Wananchi wanaoishi kandokando ya
Msitu wa Mafunzo wa Olmotonyi Mkoani Arusha wamekishukuru Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuwapatia nafasi ya kupata Kuni za kupikia pamoja
na maeneo ya kilimo hivyo kusaidia kupata kipato cha kuendesha maisha yao na
familia zao kwa miaka mingi.
Bi. Mami Lowasa akizungumza na Waandishi wa habari (Hawapo pichani) kwenye Msitu wa Mafunzo wa Olmotonyi wakati akikata kuni. |
Shukrani hizo zimetolewa na
Wananchi hao wakati wakiongea na Waandishi wa habari ndani ya msitu huo
unaomilikiwa na SUA ambao ni maalumu kwa ajili ya Mafunzo kwa Vitendo kwa
wanafunzi wanaosoma Shahada mbalimbali za Misitu katika Chuo hicho.
Akizungumza wakati akipata Kuni
za kupikia kwenye eneo ambalo linavunwa mbao kwa sasa Bi. Mami Lowasa amesema
toka azaliwe amekuta wazazi wake wakiingia kwenye msitu huo wa Olmotonyi kulima kwenye maeneo ambayo uongozi wa Kituo hicho
umekuwa ukiruhusu kufanyika kwa shughuli za kilimo.
Ukiangalia katika mji huu wa
Arusha wananchi wengi wa hali ya chini na kati wanategemea kilimo kuendesha
maisha yao lakini maeneo ya kilimo ni machache sana lakini mahusiano mazuri ya
SUA na Jamii yamewezesha wananchi wengi kupata maeneo ya kulima mazao
mbalimbali hasa mahindi, maharage na mboga ndani ya msitu huu kwenye maeneo ya
wazi yaliyovunwa mbao na yenye miti midogomidogo iliyopandwa", Alieleza Bi. Mami.
Kwa upande wake Mwananchi
mwingine Julias Sumayaki Baada ya wazazi wake wote wawili kufariki aliachiwa
wadogo zake watatu kuwatunza na kuwasomesha lakini hana kazi wala shamba ambalo
anaweza kulima kutosheleza mahitaji yake na familia hiyo aliyoachiwa na wazazi
wake.
Sina neno zuri la shukrani
ninaloweza kulisema kueleza furaha na shukrani zangu kwa uongozi wa SUA
kutokana na msaada mkubwa tunaoupata baada ya kuturuhusu kupata kuni kwenye
mabaki ya miti ambayo imevunwa, Msitu huu sisi ndio maisha yetu mimi na wadogo
zangu lakini na vijana wengi hapa mjini
alisema bwana Sumayaki.
Aliongeza kupitia msitu huu
nimeweza kupata kuni za kutumia nyumbani na wadogo zangu lakini pia zingine
kwenda kuuza Arusha mjini na kupata fedha ambazo zimeniwezesha kusomesha wadogo
zangu nilioachiwa na wazazi wangu lakini pia kupata mahitaji yangu pale pale
nyumbani, kwa kweli huu msitu ni mkombozi kwetu.
Akizungumzia mchango huo wa Msitu
wa Olmotonyi Meneja wa Kituo cha Mafunzo cha Msitu huo Bwana Said Kiparu
amesema pamoja na kutoa nafasi kwa jamii inayozunguka msitu huo kupata kuni na
maeneo ya Kilimo lakini Wananchi hao wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa katika
kutoa taarifa mbalimbali za majangili wa msitu.
Jamii inaona faida ya uwepo wa
msitu huu na wanauona kuwa ni wa kwao kwa kuwa tunawaruhusu kukata kuni hasa
matawi kwenye maeneo ambayo tumevuna magogo ya mbao lakini pia tunapomaliza
kuvuna wakati tunapanda miti mingine wao tunawapa nafasi ya kulima mazao madogo
madogo hususani viazi mviringo na mboga miti ikiwa midogo na wao wanashiriki
kuitunza wanapohudumia mazao yao alifafanua Bwana Kiparu.
Naye Rasi wa Ndaki ya Misitu,
Wanyamapori na Utalii Dkt. Agnes Sirima amesema kuwapa Wananchi wanaozunguka
Msitu wa Olmotonyi fursa ya kupata kuni na kulima ni mchango mzuri unaotolewa na Chuo kwa jamii kama
majirani wanaozunguka msitu huo.
Kwa namna hii ndio tunajenga
mahusiano mema na jamii inayotuzunguka na kuwafanya wajifunze masuala ya
umuhimu wa utunzaji misitu lakini pia kuwa walinzi wazuri wa msitu na hivyo
kupunguza changamoto za uchomaji moto tofauti na ilivyo nyanda za juu kusini
ambako majanga ya moto huaribu sana misitu mingi ya kupandwa na kuleta hasara
kwa wahusika alieleza Dkt. Sirima.
Rasi huyo wa Ndaki amesema pamoja
na kupata faida hizo lakini pia baadhi ya jamii inayozunguka msitu zimepata
ajira na wengine hufanya vibarua mbalimbali ambavyo hupata fedha za kuendesha
maisha yao huku wakijifunza pia hatua zote za upandaji, utunzaji, uvunaji na
uchakataji wa magogo ya miti na kupata mbao.
Julias Sumayaki akiongea na Waandishi wa habari wakati akikata kuni na wananchi wengine kwenye eneo la msitu linalovunwa. |
Kibao cha kuonesha unapoanzia Msitu wa mafunzo wa Olmotonyi |
Wananchi wakikata kuni wakati wa zoezi la uvunaji kwenye msitu huo likiendelea. |
Wananchi wakitoka na kuni kwenye msitu unaovunwa. |
Wananchi wakikata kuni wakati wa zoezi la uvunaji kwenye msitu huo likiendelea. |
0 Comments