SUAMEDIA

Wakulima wa mbogamboga na matunda wilayani Kilosa kunufaika na kitalu cha Raha Farm

 

Na; Gerald Lwomile

Serikali mkoani Morogoro imesema itahakikisha inawaunga mkono wakulima katika kuzalisha mazao bora ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa mbegu bora ili kuhakikisha adhma ya serikali ya kuwainua wakulima na kuwa na chakula cha kutosha inafikiwa.

 Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro Bw. Kenneth Shemdoe (kulia) akikata utepe kuzindua kitalu nyumba cha Raha Farm kushoto ni Restituta Fereta mmiliki wa kitalu hicho

Hayo yamesemwa na  Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro Bw. Kenneth Shemdoe aliyemwakilisha Afisa Kilimo Mkoa wa Morogoro wakati wa uzinduzi wa kitalu nyumba cha ‘Raha Farm’ kinachozalisha mbegu za mbogomboga na matunda kilichopo Dumila wilayani Kilosa

Shemdoe amesema wao kama mkoa wanafarijika kusikia kuwa wakulima wanaochukua mbegu katika kitalu hicho wamekuwa wakizalisha kwa tija kwani mbegu hizo za nyanya zinazozalshwa katika kitalu hicho zimekuwa na ufanisi mkubwa zinapokuwa shambani.

Kitalu cha ‘Raha Farm’

Akizungumza katika uzinduzi huo wa kitalu nyumba Mkurugenzi Mtendaji wa Kongani na Ubia (SAGCOT) Bw. Geoffrey Kirenga ambao ndiyo wamefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwezesha kitalu nyumba hicho amesema pamoja na kuwepo kwa juhudi za serikali kuhakikisha uwezeshaji unaofanywa na kongani hiyo katika kilimo unaenda nchi nzima lakini wanatamani kuona maeneo ambayo tayari wamefanyakazi yanakuwa shamba darasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kongani na Ubia (SAGCOT) Bw. Geoffrey Kirenga (kushoto aliyevaa koti) akizungumza na wakulima waliokuja kujionea kitalu nyumba hicho, wa pili kulia ni Bibi Fereta mmiliki wa kitalu

“Tunatamani kuona mambo kama haya ambayo yanaendeshwa na ‘Raha Farm’ yanakuwa shamba darasa na wakulima kutoka maeneo menginie waje kujifunza, mimi naishukuru serikali mkoani Morogoro na maeneo mengine ambao tumekuwa tukifanya nao kazi kwa kukukabali mawazo yetu ili tuweze kuchangia maendeleo” amesema Kirenga.

Akizungumza na waandishi wa habari mmiliki wa kitalu nyumba hicho cha mbogamboga na matunda Bibi. Restitua Fereta amesema tangia ameanza kujishughulisha na kilimo miaka 10 iliyopita amepata manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kujenga mtandao na wakulima mbalimbali katika mnyororo wa thamani.

Amesema yeye kama mmoja wa wanufaika wa programu ya kilimo cha Vijana yaani ‘Building a Better Tomorrow’ (BBT) ambapo Raisi wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa kiasi cha shilingi milioni 200 amekuwa akifanya juhudi kubwa kuhakikisha wakulima wengine wananufaika na utaalamu ambao yeye ameupata kutoka kwa wataalamu mbalimbali. 

“Kwa hizi mbegu za kununua kutoka kwenye makampuni ya kuuzia mbegu wakati mwingine zimekuwa na gharama kubwa, hivyo sisi tukaona tumletee mkulima suluhisho la kitalu salama, kitalu ambacho kinaweza kupunguza gharama, ambacho ukipeleka miche shambani unaweza kujua idadi yake kwa sababu tunatoa miche kwa idadi miche yetu inakuwa kwa usawa na kuanza kuzaa kwa wakati na kupata mavuno mazuri” amesema Fereta.

Kitalu nyumba hicho kilichozinduliwa kimepata ufadhili kutoka SAGCOT, TAHA na East West Seed Tanzania na Wizara ya Kilimo kitalu hicho hivi sasa kina miche ya nyanya elfu 20 ambapo mche mmoja wa nyanya huuzwa kwa shilingi mia moja na kama mkulima huyo akifanikiwa kuuza miche yote anaweza kujipatia shilingi milioni 2.










Post a Comment

0 Comments