Na: Farida Mkongwe
Taasisi ya Elimu ya kujiendeleza (ICE) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imefanikiwa kuwajengea uwezo wanakamati wa Kamati ya Ugani ya Chuo hicho ili waweze kuielewa zaidi Sera ya Ugani na kuitekeleza ipasavyo na hivyo kukiwezesha Chuo kutimiza malengo yake.
Akizungumza na SUAMEDIA katika warsha ya siku moja ya kutoa elimu kwa wajumbe wa Kamati ya Ugani ya SUA ambayo imefanyika Juni 27, 2023 chuoni SUA, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Devota Mosha amesema wajumbe wengi wa Kamati hiyo ni wapya hivyo wameona ni muhimu kuwajengea uwezo ili wayajue majukumu yao.
“Lengo letu ni kuwajengea uelewa zaidi juu ya masuala yote ya ugani yanayofanyika SUA, waelewe nini maana ya ugani Outreach na pia wajue SUA inatakiwa kutoa taarifa za teknolojia ambazo zinazalishwa na watafiti toka SUA ili ziweze kuwafikia walengwa maalum ambao wakulima, watafiti, mabwana shamba na watu ambao wanahusika na utunzaji wa maliasili katika nchi yetu”, amesema Dkt. Devota.
Dkt. Devota amesema kuwa anaamini baada ya mafunzo hayo wajumbe wa kamati hiyo watakuwa na utekelezaji mzuri katika masuala ya ugani na kwamba taarifa zinazohusu ugani katika maeneo yao ya kazi zitaripotiwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ugani na Elimu ya Kujiendeleza cha Taasisi hiyo Dkt. Emmanuel Malisa amesema mafunzo hayo yamekuja baada ya kuona wajumbe wa kamati hiyo wana uelewa tofauti kuhusu masuala ya ugani na ndipo walipoona umuhimu wa kufanyika mafunzo hayo baada ya kuruhusiwa na Menejimenti ya Chuo hicho.
“Tunaishukuru Menejimenti kwa kuturuhusu kufanya mafunzo haya sasa tunaweza kutofautisha kati ya outreach na extension na pia tunaweza kutambua vitu ambavyo ni vya outreach vinavyofanyika hapa chuoni na namna gani ya kuviripoti kutoka kwenye unit tulizopo.
Warsha hiyo imeshirikisha wawakilishi 20 kutoka Kampasi ya Edward Moringe na Solomon Mahlangu ambao wametoka katika Ndaki, Taasisi, vitengo na Vituo mbalimbali ambapo pia walipata nafasi ya kupitia Pendekezo la Muongozo wa uandikaji wa taarifa za ugani ili kila mmoja aweze kuandaa taarifa zinazotakiwa kwenye ripoti husika.
0 Comments