Na: Calvin Gwabara- Bumbuli.
Juhudi kubwa za utunzaji Msitu zinazofanywa na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kutunza kwa muda mrefu Msitu wa Hifadhi Mazumbai kumewezesha msitu huo kuwa makazi salama ya viumbe mbalimbali ikiwemo vinyonga ambao hawawezi kustahimili kuishi kwenye maeneo yenye vihatarishi kama moto na ukataji wa miti hovyo.
Hayo yamebainishwa na Mhadhiri Msaidizi na Kaimu Msimamizi wa Msitu Hifadhi Mazumbai Bw. Chamalindi Muriga wakati akieleza matokeo ya uhifadhi wa msitu huo na faida zake kwenye ikolojia ya mimea na viumbe hai msituni.
“Vinyonga hawa wenye pembe mbilli ambao hujulikana kama West Usambara two horned Chameleon na kwa kitaalamu kama ( Kinyongia multituberculata) hupatikana kirahisi na kwa wingi katika Msitu wa Hifadhi Mazumbai kwakuwa ni msitu salama na hawapati bugudha yoyote kama ilivyo kwenye misitu mingine nchini”, alieleza Mhifadhi Chamalindi.
Amesema Msitu huo wa hifadhi unaomilikiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo una ukubwa wa hektari 320, takribani ekari 800, na upo kwenye mwinuko kuanzia mita 1300 hadi 1970 kutoka usawa wa bahari na vinyonga hao hutoka wakati wa usiku muda ambao vinyonga wengi hupenda kutoka nje ya msitu na kujificha kwenye vichaka na mimea midogo ili kukwepa adui kama nyoka.
“Vinyonga hawa huvutia sana na hupenda kuonekana vizuri wakati wa usiku kwenye uoto wa mimea mbalimbali ndani ya msitu na nje ya msitu hasa kandokando mwa barabara msituni na hivyo kuwa rahisi kwa watafiti na watalii kuwaona”, alielezea Mhifadhi Chamalindi.
Aliongeza “ Hii inatokana na utulivu wa Msitu wa Hifadhi Mazumbai kuwa salama kwao kuishi na kuzaliana kwa wingi pamoja na viumbe wengine wakiwemo vinyonga na pia upekee wake ni kwamba vinyonga hupendelea maeneo yenye mwinuko mkali kuanzia mita 1200 hadi 2500 kutoka usawa wa bahari”.
Ameendelea kufafanua kuwa Idadi ya mayai ya kinyonga jike hutegemea ukubwa wa mwili wake.
Amesema baada ya mayai kuanguliwa watoto wanapaswa kujitegemea wenyewe na kuanza maisha yao na Mara nyingi kinyonga dume huwa na rangi ya kuvutia na mkubwa kuliko jike.
Pia amesema kinyonga dume ana pembe kubwa na ndefu tofauti na kinyonga jike mwenye pembe ndogo na fupi.
Katika Picha vinyonga wapatikanao katika Msitu wa Mazumbai
0 Comments