Na: Tatyana Celestine
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekubaliana kuweka ushirikiano na Taasisi za nchini India ikiwemo Taasisi ya Teknolojia India (ITI) katika maeneo mbalimbali ikiwemo Tafiti zinazohusu matatizo yanayokabili nchi hizo, Makampuni ya kibiashara, kupeleka Wanataaluma na Wafanyakazi kwenye mafunzo katika vyuo vikuu vya India ili kuweza kupata utatuzi wa changamoto zinazozikabili nchi hizo pamoja na watu wake.
Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda akitoa maelezo kwa |
Akizungumza na SUAMEDIA mara baada ya makubaliano hayo, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa Chuo kimekuliana na nchi hiyo kuwafundisha wakulima wa kitanzania njia bora za kilimo katika mazao ambayo yataleta tija kwa Serikali ya India, kuwapa uelewa wa kujua jinsi ya kuhifadhi mazao ili yanapofika kwenye soko la India yasikumbane na vikwazo vya upungufu wa ubora.
Prof. Chibunda amesema kuwa Chuo kimeamua kutilia mkazo suala la Teknolojia hasa katika mifumo ya TEHAMA na kwamba Tanzania inapaswa kuiangalia nchi ya India kama ni sehemu inayofanya vizuri katika eneo hilo hivyo Chuo kimeamua kwenda kujifunza kwao badala ya kutumia mifumo ya kununua au kupewa kutoka India pamoja na kuweka mkazo kwenye teknolojia rahisi kwa ajili ya wakulima wadogo.
“SUA kwa kuzingatia Sheria na taratibu za nchi yetu tunaweza kuwa wenyeji kwa makampuni yanayotaka kuja kufanya maonesho ya zana za kilimo, lakini vilevile sisi tukawa mabalozi wa zana za kilimo kwa watanzania na sisi kutumia hiyo nafasi kuweza kujifunza jinsi ya kutengeneza zana rahisi hasa kipindi hiki ambapo tumeimarisha Karakana yetu ya Uhandisi Kilimo”, amesema Prof. Chibunda.
Akizungumzia katika upande wa Taaluma Prof. Chibunda amesema kuwa Chuo kimetilia mkazo wanataaluma wao na kufanya wanataaluma kutoka India kuja kufundisha Chuoni hapo ili kutoa nafasi pana kwa vijana wa kitanzania kuweza kujifunza badala ya kusafirisha wanafunzi kwenda India kwa gharama kubwa.
Ameongeza kuwa Chuo kitakuwa na Program za pamoja katika upande wa wajasiliamali ili kuzalisha wahitimu watakaoweza kujiajiri, kufanya biashara kwa kuzalisha vitu mbalimbali na hivyo kuepusha changamoto ya wengine kutomaliza mafunzo yao kutokana na sababu mbalimbali.
Pamoja na hayo Prof. Chibunda amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha Vyuo Vikuu kuweza kupata fedha pia upanuzi wa miundombinu na kuangalia upya mitaala yao na kusema kuwa uhusiano ulioanzishwa baina ya Serikali ya India na SUA ni sehemu moja itakayowezesha Chuo kwenda India ili wahitimu wao waweze kuwa na umahiri.
Vilevile Chuo kwa kuzingatia mkakati wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo kitakuwa cha kuzalisha watu wanaoenda kutengeneza kazi ambapo kwasasa tayari Chuo kimeanza kwa kuwa na Atamizi, kufanya maboresho pamoja na kuweka mkazo kwa wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo ili kuendana na matakwa ya Rais kuzalisha wahitimu watakaoweza kujitegemea.
Kwa pande wake Balozi wa Serikali ya India nchini Tanzania Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema kuwa Tanzania ni sehemu muhimu ambayo inazalisha mazao mbalimbali na kwamba makubaliano waliyojiwekea yatasaidia kuimarisha masoko na kukabiliana na changamoto za ubora wa bidhaa zinazozalishwa na hivyo ujio wao umewapa fursa ya kuangalia vitu gani wangeweza kuvifanya kwa pamoja ili kuunganisha Sekta yaKkilimo, Tafiti, Masoko, Mafunzo na Teknolojia katika nchi hizo mbili.
Mhe. Pradhan ameeleza faida aliyoipata mara baada ya kutembelea baadhi ya maeneo chuoni hapo pindi alipowasili ikiwa ni pamoja na Hospital ya Taifa ya Wanyama na Kituo cha Utafiti wa Uchumi wa Bluu na kusema SUA imejidhatiti katika kuleta maendeleo ya kilimo nchini kutokana na huduma inayotoa hivyo ni wakati sasa baada ya makubaliano hayo kufanya kazi kwa pamoja kufikia malengo ya makubaliano hayo iwe faida kwa India na Tanzania.
0 Comments