SUAMEDIA

Ushirikiano SUA na TANAPA wanufaisha wanafunzi kwa vitendo

 

Na; Calvin Gwabara- Mikumi

Wahifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Mkoani Morogoro wanajivunia matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ya kuzalisha Wahifadhi bora nchini kupitia mafunzo kwa vitendo kutoka kwa Wakufunzi wake wabobevu.

Askari Uhifadhi Daraja la Kwanza katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Nicas  Nguma akizungumza na SUAMEDIA hifadhini hapo (Picha zote na Calvin Gwabara)

Hayo yamebainishwa na askari uhifadhi daraja la kwanza katika hifadhi hiyo Nicas Nguma wakati akiongea na SUAMEDIA juu ya mchango wa SUA na ushirikiano uliopo kati yake na TANAPA katika kusaidia mafunzo kwa vitendo ya wanafunzi wake.

“Ukifanya tathimini ya kina kwenye hifadhi zetu utakuta takribani asilimia 75 au zaidi ya Wahifadhi wetu ni Wanafunzi ambao wametoka SUA na hata sasa wengine wengine ambao wameajiriwa tayari wapo masomoni SUA, kwahiyo Chuo hiki kina mchango mkubwa kwenye ya uhifadhi na hii inatokana na ubora wao katika kazi kupitia mafunzo kutoka SUA” amefafanua Mhifadhi Nguma.

Aidha amesema kuwa wamekuwa wakipokea wanafunzi wa ngazi mbalimbali kutoka SUA kwaajili ya mafunzo kwa vitendo kila mwaka na kubainisha kuwa ni wanafunzi wazuri ambao watasaidia nchi katika kutunza maliasili za taifa kwani hawapati shida wanapokuwa wanawafundisha uhifadhi kwa vitendo hifadhini humo.

Kwa upande wao baadhi ya Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii wamesema katika kipindi kifupi toka waanze masomo wameweza kufahamu mambo mengi ambayo yanawafanya kupenda zaidi fani ya Uhifadhi.

 Akizunguzia mafunzo kwa vitendo wanayoyapata kwenye Hifadhi ya Mikumi mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Yassin Jafari amesema baada ya nadharia za darasani chuoni sasa wamekuja kufanya kwa vitendo huku akijivunia mbinu ya kutambua falme za wanyama na aina zake kwa ishara ikiwemo kupitia kuangalia nyayo walizokanyaga na kinyesi.

Kwa upande wake Ester Tairo amesema mahusiano mazuri kati ya SUA na TANAPA yanawawezesha kupokelewa vizuri na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wahifadhi katika hifadhi hiyo ya Mikumi kwa kushirikiana na walimu wasimamizi kutoka SUA na hivyo kufurahia mafunzo hayo wakati wote.

Mwanafunzi Yassin Jafari (wa pili kulia) akieleza anavyonufaika na mafunzo kwa vitendo huku wanafunzi akicheza mchezo wa drafti na wanafunzi wenzake wakati wa mapumziko kambinu hapo.

 ”Sisi hapa ni mwaka wa kwanza wa Shahada ya Uzimamizi wa Wanyamapori tumesoma kidogo darasani lakini sasa tumeletwa Hifadhini kwaajili ya kuona na kutenda vile tulivyofundishwa kwa vitendo kitu ambacho sio rahisi kufanywa na vyuo vingine nchini, tumepitia kwenye mafunzo yote ya uhifadhi, utambuzi wa uimea, aina za wanyama na tabia zao pamoja na ukarimu kwa wageni kwa kweli tumeiva kwa muda mfupi tu hapa tukiwa mwaka wa kwanza” ameleza Ester.

Mwanafunzi Ester Tairo akieleza yale wanayojifunza kwenye Hifadhi hiyo na faida za kusoma SUA.

Wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza wapo kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye hifadhi mbalimbali nchini ikiwemo Mikumi,Tarangire na nyingine wakijivunia mafunzo hayo huku wengine ambao hawakuwahi kuwaona wanyama hao uso kwa uso kwa mara ya kwanza.


Profesa mbobevu wa Ikolojia kutoka SUA Prof. Pantaleo Munishi akiteta jambo na kutoa maelekezo kwa wanafunzi wakati wa mafunzo kwa vitendo hifadhini

Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii SUA Dkt. Agnes Sirima akizungumza na wanafunzi hao wakati wa mapumziko hifadhini






Post a Comment

0 Comments