Na Josephine Mallango
Vyombo vya habari vimetakiwa kuendelea kuhamasisha jamii kutambua kwamba wanawake wanaweza kuongoza kihalali na kuwa viongozi bora wenye uwezo wa kielimu , kifani sambamba na kujenga hoja na siyo kwa kupendelewa.
Hayo yamejitokeza katika mafunzo ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali mkoani Morogoro yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP wakati wa mjadala shirikishi wa wanahabari na muwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Rose Ruben kutoka TGNP .
Dkt. Rose amesema kwa kipindi kirefu jamii inamuweka mwanamke kama mtu wa daraja la pili jambo linalopelekea wanawake wengi kujiona hawana thamani ya kuwa viongozi na ndio maana wao TGNP wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wanawake na waandishi wa habari ili kuweza kuleta hamasa na kuinua sauti za wanawake katika kupata usawa wa viongozi kwa jinsia zote.
Ameongeza kuwa Wanaharakati wanaamini katika uwezo wa wanawake waliopatiwa mafunzo na kupata elimu itawasaidia kuwajengea uwezo wanawake hao kwa kuwa Dhana ya uongozi kwanza inaanza na wanawake wenyewe kuwajibika na kuonesha uwezo wa kuwa viongozi.
‘’Kuhusiana na dhana nzima ya kuhitaji wanawake wawe viongozi,dhana hiyo inaanzia kwa wanawake wenyewe kuonesha uwajibikaji kwa mwanamke mwenyewe kujiinua thamani yake ya kuwa na utayari wa kuwa kiongozi ili kupata viongozi wanawake ambao wana uwezo wa kuongoza kwa hoja na siyo kwa upendeleo, wanawake hatutaki viongozi wa upendeleo tunataka Taifa liwe na viongozi wa ushindani wa kielimu, kifani au hata kuchaguliwa katika vyama vyao tueleweke vizuri hapo ‘’, amesema Dkt. Rose.
Dkt. Rose amesema pamoja na hatua ya mafanikio iliyopo ikiwepo kuongeza thamani katika Elimu kwa Serikali kuweka elimu bure kwa wote na watoto wa kike kupewa kipaumbele hata wale waliopata ujauzito baada ya kujifungua kurudi shule lakini bado Zipo mila na desturi zinazosababisha au kukataa mwanamke kugombea au kuchaguliwa na wanawake wenzie ,wanaume au na jamii yote mila hizo ndizo haswa zinazopaswa kuvunjwa
‘’ Bado kuna mila potofu zinazomkandamiza wanamke na kuona siyo kiongozi halali au hapaswi kuongoza mila hizo zinapaswa kuvunjwa kwa kuwa zinampelekea mwanamke kutojiongeza thamani na kujiona yupo yupo tu , mila hizo na mifumo hiyo kandamizi ivunjwe ndio jambo lililobaki sasa kwa kuwa kuachwa kwa mifumo hiyo kunasababisha wanamke wenyewe kujiona hawafahi au jamii kumuona hafai jambo ambalo siyo sawa kwa kuwa kila mtu ana uwezo wa kuwa kiongozi halali ‘’
Wanawake wanapaswa kuwa na uwezo wa kushiriki katika nafasi mbalilmbali za uongozi kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa kwa kushindana au kuchaguliwa kwa vigezo vya pamoja vinavyohitajika katika nafasi hiyo ya uongozi ikiwemo kushindana katika nafasi za kisiasa na kuchaguliwa kwa kuwa wana uwezo na ziada katika uongozi na kuleta maendeleo .
Wakizungumza katika mafunzo hayo wanahabari akiwemo mwanahabari Nguli Ratifa Ganzel kutoka gazeti la Uhuru amesema tatizo lililopo ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya kusambaza elimu nchi nzima hasa katika maeneo yaliyobaki korofi ya mila potofu na mifumo kandamizi ,Elimu ambayo inatakiwa kufika mpaka vijijini na kuanzia ngazi ya familia ndio iwe chanzo kwa kila mmoja kutambua wanawake wana uwezo sawa katika kuongoza na kuleta maendeleo na kwamba suala la uongozi haliangalii jinsi ya kike au kiume bali linahitaji uwezo wa kujenga hoja jambo ambalo wanawake na wanaume wana haki sawa ya kuchagua au kuchaguliwa na kuongoza .
0 Comments