Na; Gerald Lwomile
Kufuatia kuwepo kwa gharama
holela za ujenzi wa barabara nchini, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi
(NCC) imeamua kuandaa miongozo ya msingi itakaohakikisha inakidhi bajeti ya
taifa inayoandaliwa kwa mwaka na kuhakikisha barabara zinazojengwa au
kukarabatiwa zinakuwa na ubora unaostahiki.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi Mhandisi Dkt. Matiku Mturi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) |
Hayo yamesemwa Juni 20, 2023 na
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi Mhandisi Dkt. Matiku Mturi,
wakati akiongea na waandishi wa habari mjini Morogoro kwenye kikao kazi cha
wadau wa barabara.
“Kila Serikali inapotaka kujenga
mradi wowote inakuwa na bajeti, yale makisio ya bajeti kwa kiasi kikubwa
yanatokana na gharama za ujenzi wa kilometa moja ya barabara ‘unit cost’ na ile
kilometa moja inajengwa kwa kiasi gani inapatikana kwa kuwa na gharama za
ujenzi au ukarabati wa kazi moja moja ambazo zinapelekea kujenga hiyo kilometa
moja ‘unit rates’ kwa hiyo hii ni kazi ya msingi kujua gharama za ujenzi”
amesema Dkt. Mturi
Amesema pamoja na kufanya kazi
hiyo ya kutengeneza muongozo wa gharama lakini wanatambua kuwa barabara hizo
zinaweza kutofautia kwani zipo ambazo zinaweza kubeba magari makubwa yenye
uzito mkubwa na zile za kawaida kulingana na matumzi ya barabara husika.
Dkt. Matiku amesema mara baada ya
kazi hiyo kukamilika wanatarajia kuona makandarasi wanapata ushindani wa
kihalali kwani kuna wakati wakandarasi wasio na viwango huweka bei ndogo ili kuwapa
zabuni na matokeo yake kazi inafanyika chini ya viwango
Naye Afisa Ujenzi Mkuu wa Baraza
la Taifa la Ujenzi Mhandisi Tumaini Lemunge amesema sasa hivi kumekuwa na mkanganyiko
wa bei kwa wakandarasi na kila mkandarasi amekuwa akija na bei yake ya ujenzi wa
barabara kwa kilomita moja ili ashinde zabuni.
Afisa Ujenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi Mhandisi Tumaini Lemunge akifafanua jambo kwa waandishi wa habari |
Amesema kutokana na bei hiyo
elekezi itakayopatika itakuwa ni rahisi kupata wakandarasi wenye viwango na
watakaofanyakazi kwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na ujenzi bora wa barabara
Naye Mhandisi Perpetua Kisamba kutoka Wakala ya Barabara (TANROADS) amesema hatua hiyo iliyochukuliwa na Baraza la Ujenzi la Taifa itawarahishia kazi kwa kupata wakandarasi wenye viwango, tofauti na awali ambapo Mkandarasi mwenye bei ndogo ndiye alipewa nafasi ya kujenga barabara huku baadhi yao wakishindwa kuwa na viwango bora vya kazi au kushindwa kumaliza ujenzi kwa wakati.
Mhandisi Perpetua Kisamba kutoka Wakala ya Barabara (TANROADS) |
Kikao kazi hicho kimeshirikisha Wizara ya Ujenzi, Fedha, Tamisemi, Wakala ya Barabara, TRC, TARURA na Wakandarasi.
Pichani chini Wadau wa barabara wakijadili mambo mbalimbali katika kikao kazi
0 Comments