SUAMEDIA

Serikali kuzipatia shule vifaa na walimu ili kutoa mafunzo ya Amali

Na; Amina Hezroni - Morogoro

Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imekutana na wakuu wa shule za Sekondari za Ufundi Tanzania ili kufahamu gharama halisi za utekelezaji wa Mitaala Mipya ya Elimu itakayokuwa ikihusisha uwepo wa Mafunzo ya Amali ili kuhakikisha shule hizo zinakuwa na vifaa na walimu wanaohitajika ili kuweza kutoa mafunzo vizuri.



Mkutano huo umefanyika mkoani Morogoro ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mitaala, Prof. Makenya Makobo na Mwenyekiti Kamati ya Sera Prof. Joseph Semboja pamoja na wakuu wa shule zote za sekondari zinazotoa mafunzo ya Uhandisi, Kilimo, Mapishi,Ususi na Fani nyingine.

Akizunumza katika mkutano huo Prof. Nombo amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuboresha Mitaala na tayari wameshapokea maoni ya wadau ya namna ya kuboresha Mitaala hiyo ambapo wengi wametamani watoto wanapomaliza kidato cha nne, cha sita, Chuo Kikuu au darasa la saba wawe na ujuzi wa mikono utakaowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

“Vilevile ni maelekezo ya Mh. Raisi kwamba ni lazima wahitimu wetu wawe na ujuzi wa kujitengemea hivyo mabadiliko yaliyofanyika kwenye Mitaala ni kuhakikisha kwamba katika ngazi zozote za elimu wanafunzi wanapata ujuzi au Amali  kwahiyo sasa katika mpango wetu wa utekelezaji wa Mitaala hiyo mipya inayopendekezwa tumeona ni vyema tuingie katika hatua za utekelezaji wa Mitaala hiyo”, amesema Prof Nombo. 

Prof Nombo ameeleza kuwa mitaala ya awali ilikuwa haina Amali kwa upande mkubwa lakini sasa wakwenda kuona Amali ikiwa sehemu kubwa ya mafunzo kwenye Sekondari hivyo wamewaita walimu Wakuu wa Shule zote ambazo zipo katika Mfumo wa Elimu ambao tayari unatoa mafunzo ya Amali kueleza hali halisi ya shule zao zilivyo ili kuweza kuingiza katika mahesabu ya gharama za utekelezaji wa mtaala huo pamoja na kuweza kujua namna nyingine ya kufundisha. 


Aidha Prof. Nombo amewataka Walimu Wakuu, Wazazi pamoja na wanafunzi ambao watakwenda kusoma katika shule hizi watambue hawatakuwa na muda mwingi sana madarasani watakuwa na muda mwingi katika Kalakana na Shambani ili kuweza kujifunza kwa vitendo ili kutoka na Amali zitakazomuwezesha kufanya kazi. 

“Wazazi watambue kuwa huu ni muelekeo mpya wa elimu ambapo tunataka kutoa watanzania ambao wanauwezo wa kufanya kazi tofauti na ilivyokuwa zamani, walikuwa wana ujuzi wa nadharia sasa tunatamani wawe na ujuzi wa nadharia kidogo na ujuzi wa kufanya kazi kwa wingi”, amesema Prof Nombo.

Kwa upande wake mmoja ya wakuu wa Shule kutoka shule ya Sekondari Bwiru Boys Mwl. Thomas Werema ameishauri Serikali kuwazawadia dhana za kufanyia kazi wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ili wakaweze kujiendeleza zaidi wanapomaliza mafunzo yao.

Aidha Makamu Mkuu wa Shule Ifunda Sekondari Mwl. Yona Mwakalango ameishauri Serikali kutoa elimu zaidi kwa walimu na wazazi ili waweze kuhamasisha watoto wao kwenda kusoma katika Vyuo vya Ufundi lakini pia  ameiomba Serikali kuendeleza vipaji vya watoto vinavyotambuliwa shuleni ili teknolojia wanazozigundua ziweze kuwa na manufaa katika jamii. 








Post a Comment

0 Comments