Na Hadija Zahoro
Viongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakiwemo Wakuu wa Idara, Ndaki na Vitengo mbalimbali wamepata fursa ya kupewa mafunzo kuhusu VVU/UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY) na Unyanyasaji wa Kijinsia mahala pa kazi lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto mbalimbali za magonjwa zinazotokana na mfumo wa sasa wa maisha.
Akizungumza katika Semina hiyo iliyofanyika Chuoni hapo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali kupitia Waraka wa Utumishi namba mbili wa 2014, kuhusu Udhibiti wa masuala hayo na kufadhiliwa na mradi wa HEET.
Prof. Mwatawala ameeleza kuwa ugonjwa wa UKIMWI ni agenda kubwa ya Chuo cha SUA na umeendelea kuwa tatizo kubwa la Afya Duniani ambapo tangu kuanza kwa tatizo hilo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu Milioni 74.6 wameshambuliwa na VVU na watu Milioni 32 wameshafariki Dunia kwa UKIMWI.
Amesema kuwa kasi ya maambukizi kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 ni asilimia 11.2 ambapo kundi kubwa ni la wanafunzi waliopo vyuoni na asilimia 80 wapo katika hatari ya kuambukizwa Virusi vya Ukimwi.
Ameongeza kuwa ugonjwa wa UKIMWI umechangia madhara makubwa na mengi katika jamii tangu kuzuka kwake na hakuna mtu ambaye hajawahi kuguswa na tatizo hili aidha moja kwa moja au kwa mtu wake wa karibu
Akielezea hali halisi ya Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY), Prof. Mwatawala amesema kuwa awali magonjwa haya yalipatikana zaidi katika nchi zilizoendelea hali iliyosababisha yaitwe magonjwa ya matajiri lakini kwa sasa imekuwa kama hali ya kawaida kutokana na kuathiri watu wa hali yoyote ile.
‘‘Kwa mujibu wa ripoti ya WHO mwaka 2008, magonjwa sugu yasiyoambukiza yalisababisha vifo milioni 36 Duniani kote sawa na asilimia 63 ya vifo vyote ambapo kati ya vifo hivyo, asilimia 48 vilichangiwa na magonjwa ya moyo na magonjwa mengine kama vile kisukari, saratani na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa’’, ameeleza Prof Mwatawala.
Kwa upande wa Afya ya Akili, Prof Mwatawala ameeleza kuwa kwa Tanzania pekee takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa mtu mmoja kati ya wanne anakabiliwa na afya ya akili hivyo, ametoa rai kuwa wanajumuiya wa SUA wanapaswa kupewa ufahamu kuhusu magonjwa ya afya ya akili, umuhimu wa tiba na ushauri wa kisaikolojia ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Amesisitiza kuwa takwimu hizo hazijatolewa kwa ajili ya kutisha bali ni kwa ajili ya kuonesha hali halisi ya maambukizi ili kuweza kujikinga.
0 Comments