SUAMEDIA

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K Nyerere cha Kilimo na Teknolojia - BUTIAMA (MJNUAT) vimetia saini ya Hati ya makubaliano kubadilishana Mitaala

Na: Tatyana Celestine

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) pamoja na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K Nyerere cha Kilimo na Teknolojia - Butiama  (MJNUAT) vimetia saini ya Hati ya Makubaliano katika kubadilishana Mitaala na Wahadhiri ikiwa na lengo la kuhakikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza lengo lake la kukuza elimu ya juu nchini kama maelekezo yalivyotolewa na Waziri ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolph Mkenda alipoagiza Chuo cha Butiama  kianze ifikapo Nov, 2023.

Wakuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) pamoja na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Kilimo na Teknolojia - Butiama  wakitia saini ya Hati ya makubaliano katika kubadilishana Mitaala na Wahadhiri leo.

 

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) June 9, 2023 Mgeni rasmi  ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa maelekezo ya Waziri wa Elimu na utiaji saini wa Hati ya Makubaliano yanakifanya Chuo cha Mwalimu Julius K Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kuweza kujidhatiti ikiwa ni sehemu ya kufikia vigezo vya kutoa elimu bora ili vijana wa kitanzania wapate fursa ya kusoma katika chuo hicho.

 Aidha Prof. Nombo amesema kuwa ushirikiano uliooneshwa na vyuo hivyo viwili mpaka kufikia kuweza kubadilishana mitaala na wahadhiri ni dhahiri SUA itakuwa mlezi wa chuo hicho hivyo amewataka MJNUAT kuendelea na mchakato wa kukamilisha mitaala yao na kupata Ithibati kutoka TCU kwani makubaliano yaliyofanyika ni kuwawezesha kuanza kutoa mafunzo hivyo wasimamie vema ili kupata program zao wenyewe zenye Ithibati ambazo zipo chini ya Chuo chao ili kusaidia kuongeza ubora na udahili wa wanafunzi katika nyanja hizo.

 Katibu Mkuu huyo amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu nchini kwa mwaka 2023/2024 kwa kudahili wanafunzi wapatao 133,000 kwa mwaka wa kwanza wanaotarajia kujiunga na kuongeza mpango wa udahili wa wanafunzi wa kike kupitia mpango wake wa kuongeza fursa za ziada kwa wanafunzi wanawake katika program za sayansi kama vile Samia scholarship kuweza kuhamasisha wanafunzi wa kike kujiunga katika program za sayansi na tiba hivyo wanafunzi takribani 700 ni wanufaika wa mpango huo.

 Akizungumza mara baada ya utiaji saini Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa  pamoja na changamoto walizopitia kuandaa mtaala lakini SUA ipo tayari kushirikiana na Chuo Kikuu cha Butiama kwa hali na mali hivyo imeonelea ni vema kutoa mchango wake kusaidia chuo hicho kianze kwani tayari wao ni washirika wa muda mrefu na wala hawashindani zaidi wataongeza fursa kwa vijana wa kitanzania kupata elimu ya juu ya chuo kikuu kama ilivyokwishafanya kwa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU) zaidi ya miaka kumi na mwaka 2023 wanategemea kuanzisha Shahada ya pamoja.

 Nae Mkuu wa Chuo cha Mwalimu  K Nyerere cha Kilimo na Teknolojia Butiama  Prof. Lesakit Millau amesema kuwa uamuzi wa makubaliano kati ya SUA na Butiama  ni wa manufaa kwa nchi ya Tanzania na Serikali imeipa umuhimu  kwa kutenga fedha kiasi cha sh. bilioni 2.66 kukiwezesha kuanza kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoko kukiwezesha chuo hicho kufanya udahili ifikapo Nov 2023.

 Prof. Millau ameongeza kuwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Chuo chao kimepata kiasi cha shilingi Bil. 102 ambapo Chuo hicho kitajenga Ndaki ya Kilimo, Shule Kuu ya Uhandisi Kilimo na Teknolojia ya Umwagiliaji, Shule Kuu ya Uandisi na Teknolojia ya Uchimbaji Madini na Nishati mbadala pamoja Shule Kuu ya TEHAMA na Biashara itakayojengwa Kampasi ya Tabora na kufanya chuo kuweza kudahili wanafunzi 6,200.

 Akikamilisha zoezi hilo Naibu Waziri na Mbunge wa Butiama Mh. Jumanne Sagini amepongeza ushirikiano huo wa kupelekea utiaji saini wa Hati ya makubaliano katika kubadilishana mitaala na wahadhiri pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kuharakisha mchakato huo kukamilika kwa haraka tangu alipoingia madarakani 2021  na kufanya chuo hicho kuanza mwezi Nov 2023 pia kufanya Butiama kupata hadhi tofauti na awali.

 Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Caroline Nombo, Naibu Waziri na Mbunge wa Butiama  Jumanne Sagini, wakuu wa Chuo SUA pamoja na MJNUAT na viongozi wengine mbalimbali.

 

Wakuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) pamoja na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K Nyerere cha Kilimo na Teknolojia - Butiama wakipena mikono mara baada ya kutia saini ya Hati ya makubaliano katika kubadilishana Mitaala na Wahadhiri leo.

 

 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda
akizungumza mara baada ya utiaji saini ya Hati ya makubaliano katika kubadilishana Mitaala na Wahadhiri
  

Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Kilimo na Teknolojia Butiama  Prof. Lesakit Mellau akizungumza mara baada ya utiaji saini  ya Hati ya makubaliano katika kubadilishana Mitaala na Wahadhiri


 Viongozi wengine mbalimbali wakishuhudia utiaji saini ya Hati ya makubaliano katika kubadilishana Mitaala na Wahadhiri


Katika picha ya pamoja  mara baada ya Utiaji saini ulioshuhudiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo,(wa kwanza kushoto waliokaa) Naibu Waziri na Mbunge wa Butiama Jumanne Sagini,(katikati waliokaa), Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda (wa kwanza kulia waliokaa) pamoja na viongozi wengine.




 

 

Post a Comment

0 Comments