Na; Hadija Zahoro
Mawasilisho ya tafiti
mbalimbali kutoka nchi za nje pamoja na tafiti kutoka taasisi za ndani ya nchi ikiwemo SUA, zimesaidia kuonesha njia mbadala za kutatua
changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kurudisha uoto wa asili kwa
kutumia sayansi za wananchi, sayansi ya kitaalamu ya utambuzi wa miti ya asili
pamoja na mimea ya uoto wa asili kwenye vyanzo vya maji zitakazosaidia
kuboresha mazingira bora kwa maendeleo endelevu nchini.
Washiriki wa Kongamano la siku mbili kwenye wiki ya Kumbukizi ya 18 ya Sokoine wakiwa katika picha ya pamoja |
Hayo ameyasema Prof.
Japhet Kashaigili, Mratibu wa utafiti na machapisho katika Kurugenzi ya
Uzamili,Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na
Ushauri wa Kitaalamu wakati akizungumza na waandishi wa habari Mei 24, 2023 katika Kongamano la siku mbili kwenye wiki ya Kumbukizi
ya 18 ya Sokoine iliyolenga kuzungumzia suala la mazingira wezeshi kwa ajili ya
kilimo.
Prof. Kashaigili amesema tafiti
zilizowasilishwa katika Kongamano hilo zimeonesha kuwa shughuli za binadamu ikiwemo
kukata miti, kilimo kisicho rafiki na mazingira pamoja na ufugaji holela ni viashiria vikubwa vinavyopelekea
changamoto ya mabadiliko ya
tabianchi na kukwamisha maendeleo
endelevu nchini.
Ameeleza kuwa uoto wa
asili unapotolewa inaruhusu kusambaa kwa hewa ya ukaa inayopelekea kuharibu tabaka
la anga na baadae kuongezeka kwa joto duniani hivyo, ikitumika njia ya
kurudisha uoto wa asili kwenye vyanzo,
inaweza kusaidia kuongeza uwezo wa maji kuvivia chini ya udongo na kupunguza uzalishaji wa udongo
unaotiririka kwenye mito na kusababisha
athari kwenye ikolojia ya mito na
mabwawa.
“Nikichukulia mfano wa
bwawa la Mtera, Kidatu pia nikichukulia mfano jitihada kubwa ya nchi
kwenye Mradi wa Mkakati wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, utaona kwamba kama
hatuwezi kupunguza kwa kutumia njia hizi mbadala za kupunguza uzalishaji wa
udongo inawezekana tukaathiri maisha ya bwawa baada ya kujaa tope”, ameeleza Prof. Kashaigili.
“Matokeo ya tafiti
yametuonesha kuwa tukiweza kufanya
vizuri kwenye urudishaji wa uoto wa asili
tunaweza tukapunguza uzalishaji wa tope
ambalo linaenda kwenye mabwawa na kuongezea uwezo wa maji kuvivia kwenye
udongo ambayo ni faida wakati wa kiangazi katika maana ya kuongezea uwepo wa
maji wakati wa kiangazi”, ameongeza Prof. Kashaigili.
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi katika Idara ya Mimea na Vipando na Mazao ya
bustani, Bi.Caroline Maro, ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinawapatia wanataaluma wake fedha kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali ambazo
baadae zinakuja kutoa majibu au
suluhisho ya changamoto zinazoikabili nchi hasa kutokana na madaliko ya tabia
nchi.
Amesema kuwa yeye ni mmoja
wa Mwanataaluma aliyenufaika na fedha zilizotolewa katika miradi na anafanya utafiti wa kuangalia ni jinsi
gani wanaweza kuboresha vyakula au kuongeza vyakula vyenye virutubisho
vinavyoweza kuepukana na matatizo ya afya hasa upungufu wa madini na vitamini
katika Mikoa ya Nyanja za Juu Kusini.
0 Comments