Na: Adam Maruma – Morogoro.
Imeelezwa kuwa Hali ya vyanzo
vingi vya mito hapa nchini si ya kuridhisha kutokana na shughuli mbalimbali za
kibinadamu zinazoendelea katika vyanzo hivyo
huku baadhi ya vyanzo vikiwa katika
hali nzuri na endelevu.
Hayo yameelezwa na Prof. Japhet
Kashaigili ambae ni Mratibu wa Utafiti na Machapisho kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA wakati
akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya
Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa na Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake
la Mazingira UNEP kila ifikapo June 5 ya
kila mwaka.
Prof. Kashaigili amezitaja shughuli
zinazoharibu vyanzo hivyo ni pamoja na Ukataji miti, shughuli za Kilimo,
Ufugaji, Uchomaji mkaa na Uanzishwaji wa makazi ya watu kiholela kuwa tishio
kubwa la vyanzo hivyo.
‘’Hali ya vyanzo vingi vya mito
mingi si vya kuridhisha huku baadhi ya vyanzo hivyo ikiwa ni nzuri na endelevu
na hii inategemea maeneo vyanzo hivyo
vilipo na watu wanaozunguka vyanzo hivyo ni watu wa aina gani na wanafanya
shughuli gani, mito mingi ukiangalia inaanzia
milimani na ndiko kuna shughuli za kibinadamu huko, kwa kuwa mvua zinanyesha zaidi
ukilinganisha na maeneo mengine’’, amesema
Prof. Kashaigili.
Mtaalam huyo wa masuala ya
Mazingira ameongeza kuwa amekuwa akifanya tafiti nyingi kwenye eneo la maji na
mazingira kwa muda wa zaidi ya miaka 20 na kusema kuwa ukataji miti na hasa miti ya asili ambayo
huondoa uoto wa asili ambao huhifadhi
mito kwa kuifunika mito hiyo ili kuendeleza uasili wake na hivyo ukataji huo wa
miti ya asili na mimea mingine imekua na athari kubwa kwa vyanzo vingi vya mito
pamoja na vyanzo vingine vya maji.
Aidha Prof. Kashaigili amezitaja
athari nyingine za shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya mito au kando ya
mito hiyo kuwa ni pamoja na kubadilika kwa mwenendo wa maji ya mito kwa
kutawanyika ovyo na kuacha njia yake asili ambayo hupelekea kiasi cha maji na
misimu ya maji kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa tope
katika njia ya mito hiyo.
‘’Nimekuwa nikifanya tafiti nyingi kwa zaidi ya miaka 20 kwenye eneo la maji na athari zingine zinasabishwa kwa kiasi kikubwa na aina ya kilimo kama kilimo cha vinyungu, kinachofanyika kwenye vyanzo vya mito au pembeni mwa mto pamoja na shughuli nyingine zinazohusisha ukataji miti, hasa miti ya asili ambayo huhifadhi mto kwa kuifunika ili kuendeleza uasili wake sasa ukatiji wa miti hiyo ni kama kuifunua mito hiyo na kuiweka wazi na hii inasababisha maji mengi kupotea na pia kupelekea mto kupoteza mwelekeo wa asili wa maji na kupelekea kiasi na misimu ya maji kupungua kwa kiasi kikubwa’’, Prof. Kashaigili.
Mtafiti huyo nguli wa masuala ya
mazingira na maji ameongeza kuwa uwezo
na uhifadhi wa maji kwenye mito wakati
wa kiangazi inategemea aina ya uoto uliopo katika maeneo yanayozunguka vyanzo
vya mito na kusema kuwa kama eneo hilo lina kiasi kikubwa cha miti iliyokatwa
inayopelekea uwezo wa kuhifadhi na kunywea kwa maji kwenye udongo kwa haraka, kwa
sababu dakio la maji linakua halina uwezo wa kuhifadhi maji kwa muda mrefu
kutokana na athari za shughuli zinazofanyika katika maeneo yaliyo karibu na mto
huo na maji kuwa machache kipindi cha kiangazi na wakati mwingine kuisha
kabisa.
Amezitaja baadhi ya maeneo yenye
uhifadhi mzuri wa vyanzo vya mito kuwa ni mto Zigi uliopo katika bonde la mto
Pangani mkoani Tanga, bonde la Mbarali liliopo mkoani Mbeya ambapo bonde la mto
Mbarali amelitaja kama eneo ambalo bado uhifadhi wake si wa kuridhisha
ukilinganisha na viwango vinavyokubalika lakini jitihada zinazofanyika na
mwamko zinaonesha mwanga katika siku zijazo.
Prof. huyo ameitaka jamii
kuchukulia suala la utunzaji wa mazingira kuwa la kila mmoja kwa kuzifanya
shughuli zao za kila siku ziwe rafiki kwa mazingira kwani mazingira yakitunzwa
vizuri na yenyewe yataitunza jamii na pia ameshauri kubuniwa kwa shughuli
mbadala kama ufugaji nyuki, uanzishwaji wa bustani na kilim0 cha miti ya
matunda kama mbadala wa shughuli zinzopelekea uharibifu wa mazingira.
0 Comments