Na: Winfrida Nicolaus
Idadi ya
Wahitimu katika Mahafali ya katikati ya mwaka kwa masomo (Mid-year Graduation)
katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeongezeka kutoka Wahitimu 209
kwa mwaka 2022 hadi 274 kwa mwaka 2023 ambapo kati ya hao watunukiwa wanawake
ni 91 sawa na asilimia 33.2 ya wahitimu wote.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda akizungumza katika mahafali ya katikati ya mwaka wa masomo |
Amebainisha
hayo Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda wakati akitaja takwimu za
Wahitimu katika Mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Michezo vya
Kampasi Kuu ya Edward Moringe ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali
akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambapo amesema
katika Mahafali hayo ya katikati ya mwaka zipo jumla ya Program 56 za masomo
zenye jumla ya Wahitimu 274 wakiwemo wanaume 183 na wanawake 91.
Katika
takwimu hizo wahitimu 189, ni kutoka Shahada za Kwanza ambapo wanaume ni 131,
na wanawake 58, Shahada za Umahiri wahitimu 48 wanaume 24, na wanawake 24,
Stashahada ya Juu ya Elimu wahitimu 2 wote wakiwa ni wanaume, Shahada za Uzamivu
15, wanaume 10 na mwanamke 5, wahitimu wa Stashahada 18 wanaume 14 na wanawake
4 vilevile wahitimu 2 wa Astashahada wote wakiwa ni wanaume.
Aidha, Prof. Chibunda amesema kuwa
wanastahili kujipongeza kwa mafanikio ambayo wameendelea kuyapata kila mwaka ya
kuongeza idadi ya nguvu kazi na yenye Taaluma stahiki katika nchi ya Tanzania
ambapo mafanikio hayo yanatokana na ufanyaji kazi mzuri wa Viongozi wa Chuo, Wahadhiri
na wafanyakazi wote wa Chuo hicho ambao wamewezesha kupiga hatua zaidi mwaka
hadi mwaka.
Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba (aliyekaa katika kiti kikubwa katikati) akiwa katika zoezi la kutunuku shahada mbalimbali katika mahafali |
Vilevile ametoa pongezi maalum kwa wahitimu
wote ambao wametunikiwa Shahada zao katika Mahafali hayo na kusema kuwa yote
hiyo ni kutokana na nidhamu na bidii zao ambazo ndio siri za mafanikio katika
kutafuta Elimu, hivyo amewaasa kuendelea kuwa na bidii, uaminifu na moyo wa
kujituma waliokuwa nao wakati wa masomo kuendelea nao sehemu zao za kazi ili
waweze kufanikiwa zaidi kukitangaza chuo vizuri.
‘‘Mahafali ni tukio la kipekee sana kokote
pale duniani, kwa wahitimu tukio hili ni muda mahususi kwa kusheherekea na
kutathmini miaka kadhaa waliotumia katika kuhakikisha wanafikia malengo yao
aidha baadhi ya Mahafali ni muda kwa wahitimu kutafakari kuingia katika
ulimwengu wa Ajira na ujenzi wa Taifa”, ameeleza Prof. Chibunda.
Ameongeza kuwa Chuo kimeendelea kutekeleza
malengo na majukumu yake kupitia katika Ndaki zake zote saba (7), Shule Kuu ya
Elimu, Kurugenzi na Taasisi zake tangu Mahafali ya 40 Novemba 2022 ikiwemo
utekelezaji wa shughuli za mafunzo ambazo zimeendelea kufanyika chuoni hapo
kama ilivyopangwa katika Kampasi zote tatu kwa maana ya Edward Moringe, Solomon
Mahlangu pamoja na Kampasi ya Katavi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, amesema
takribani miezi sita tangu kufanyika kwa Mahafali ya 40 katika kipindi hicho
Baraza limetekeleza majukumu yake makuu kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kusimamia
Menejimenti ya Chuo ili itimize majukumu ya chuo ambayo ni kutoa Mafunzo,
kufanya Tafiti, kutoa Huduma za Kitaalam na Ugani vilevile kuzalisha Mali.
Pichani chini ni matukio mbalimbali katika mahafali
0 Comments