Na; Gerald Lwomile - Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge
na Uratibu imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuhakikisha
kinafanyakazi pamoja na Serikali na kutumia tafiti na rasilimali zake kunufaisha wananchi
katika sekta mbalimbali ikiwemo namna ya kujiandaa kukabiliana na majanga.
Akizungumza Juni 30, 2023 wakati
wa uzinduzi wa Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano la Kidigitali la Afya Moja,
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi
amesema SUA ikishirikisha na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa
imekuja na mfumo bora wa utoaji taarifa kidijitali na kurahisisha kukabiliana
na majanga yanayoweza kujitokeza.
Dkt. Yonazi amesema vyuo vikuu
nchini ikiwemo SUA vinao wajibu mkubwa katika kufanya tafiti kwa kushirikiana
na taasisi mbalimbali ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kwani kwa kufanya
hivyo kama taifa litakuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na maafa yakiwemo ya
moto, magonjwa ya mlipuko na majanga mengine mbalimbali.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi akifafanua kuhusu umuhimu wa Afya Moja |
“Tumeshaona ongezeko la wananchi,
tunaona mabadiliko ya teknolojia je mifumo hii itadumu kwa muda gani? au kuna
mifumo mingine tunaweza kuitafuta au kuitengeneza ikatusaidia katika kituo
chetu, huenda kituo hiki kikazaa vituo vingine, changamoto hii niitoe kwenu
nyinyi wataalamu lakini pia kwa vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama” amesema
Dkt. Yonazi
Awali akikabidhi Mradi huo wa
Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano la Kidijitali la Afya Moja, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda amesema uwepo wa Jukwaa
hilo utaimarisha uwezo wa nchi katika kubaini uwepo wa viashiria vya majanga yanayoweza
kudhuru afya ya binadamu ikiwemo magonjwa ya mlipuko na matukio mengine na kuyatolea
taarifa kwa wadau.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda (aliyesimama) akitoa maelezo ya utekelezaji wa Jukwaa hilo, aliyekaa ni Dkt. Jim Yonazi |
“Katika kuhakikisha Jukwaa hili
linafanya kazi kama lilivyokusudiwa, Chuo chetu kilitoa vifaa vya tehema ili
kufanikisha huu mradi, vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 42.3 kwenye
hivyo vifaa kuna seva 1, kifaa cha huduma kwa wateja na komputa 8” amesema Prof.
Chibunda.
Akitoa taarifa ya mradi huo Afisa
Tehema Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Alex Ndimbo amesema endapo
jukwaa hilo litatumika kikamilifu litaimirisha sehemu ya Afya Moja na wizara za
kisekta katika uwezo wao wa kutambua matukio ya ugonjwa pamoja na ishara na
taarifa za awali zinazohusiana na chanzo cha ugonjwa au tukio lolote kijografia
au kijiorojia na kuchakata takwimu hizo mapema ili kutoa tahadhari ya mapema
katika kuratibu kabla ya kutokea mlipuko mkubwa wa ugonjwa au madhara yoyote
kwa jamii.
Amesema kupitia jukwaa hili
wananchi wataweza kutoa taarifa mbalimbali za maafa kwa njia ya kupiga simu,
ujumbe mfupi na hata ‘WhatsApp’ na hivyo kurahisisha namna ya
kukabiliana na majanga.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia Mradi wa ‘Sacids Foundation’ kimeshirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu katika kuhakikisha Jukwaa hilo Shirikishi la Mawasiliano la Kidigitali la Afya Moja kwa kutoa vifaa, kiteknolojia na ufundi.
Picha juu ni wadau mbalimbali katika uzinduzi wa Jukwaa hilo
0 Comments