Na Nicholus Romani
Watafiti wa masuala ya lishe wametakiwa kurejesha matokeo ya tafiti zao kwa jamii kuhusiana na majibu waliyoyapata katika utafiti wao ikiwa ni pamoja na kuieleza jamii nini wafanye ili kuboresha afya zao na kipi wasikifanye kwa lengo la kulinda afya zao.
Picha kwa hisani ya The Tanzania Academy of Sciences - TAAS |
Akizungumza na SUA Redio kupitia kipindi cha Kapu la Leo, Prof. Joyce Kinabo kutoka Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Mlaji ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amesema kutokana na Matokeo ya Ripoti ya Utafiti wa Kidemografia na Afya Tanzania ya 2022 iliyofanyika kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu wamegundua ongezeko kubwa la ugonjwa wa utapiamlo kwa baadhi ya mikoa.
“Ofisi ya Taifa ya Takwimu imefanya utafiti na kuona kuwa baadhi ya mikoa kama vile Iringa, Rukwa , Kagera , Njombe , Geita na Songwe ina idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa wa utapiamlo kwa hiyo jamii inatakiwa kupewa elimu namna gani ya maandalizi ya mapishi na matumizi bora ya vyakula vilivyomo katika maeneo yao.
amesema licha ya mikoa hiyo kuwa na vyakula vingi na mbogamboga za kutosha lakini bado watu wazima na Watoto wanasumbuliwa na ugonjwa wa utapiamlo katika maeneo yao wanayoishi kutokana na kutumia aina moja ya chakula pia kushindwa kujua jinsi ya kuandaa matokeo yake kukosa virutubisho vinavyotakiwa.
Aidha, Prof kinabo ameeleza kuwa wataalamu wanatakiwa kutoa elimu bora ya namna ya matumizi na mapishi bora ya vyakula ambavyo vinatumika kuanzia kwa mama mjamzito pia kwa mtoto mchanga na hata kwa watu wazima hiyo itasaidia jamii kuelewa namna bora ya kuandaa na kupika vyakula vyao ili kuongeza lishe mwilini.
“Watu wanatakiwa kuwa na mazoea ya kula vyakula tofauti tofauti hata kama chakula kikuu maeneo hayo ni viazi basi wanatakiwa japo kuweka ratiba ya kula kwa kiasi viazi na mboga za majani , maharage au kunde , Samaki , maziwa , mayai , nyama pia na matunda tofauti tofauti ili kupunguza ongezeko la ugonjwa wa utapiamlo katika kaya”, ameeleza Prof. Kinabo.
Pia,amewaasa wataalamu kuwasisitiza mama wajawazito kutumia vyakula ambavyo wanatakiwa kula na kuacha vile vinavyohatarisha afya zao ili viweze kumjengea afya bora yeye Pamoja na mtoto aliye tumboni.
Prof. Kinabo amewataka wazazi kuzingatia muda wa kuwanyonyesha watoto kuanzia pale wanapozaliwa angalau kwa miezi sita kwani maziwa ya mama yana faida katika kumuepusha mtoto na udumavu wa akili.
0 Comments