Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Timu ya Watafiti na Wataalamu
wabobevu wa masuala ya lishe nchini wakiongoza na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
wakutana kwenye mafunzo ya siku nne kuwajengea uwezo kabla ya kuanza zoezi la Kitaifa
la kufaya tathimini ya haraka ya visababishi na viashiria vya utapiamlo na udumavu
katika mikoa nane ya Tanzania.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Mwita Waibe akifungua Mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu OR TAMISEMI. |
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi
Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Mwita Waibe
amesema kazi hiyo waliyopewa kikosi kazi hicho cha kitaifa ni matokeo ya
dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kutaka kupunguza na kumaliza kabisa tatizo la utapiamlo na udumavu nchini
kupitia utafiti wa kina na majibu atakayokabidhiwa na kikosi kazi hicho.
“Katika Mjadala wa Marais ambao una
Marais zaidi ya kumi wa Afrika Rais wetu amepewa jukumu la kuwa kiongozi wa
timu hiyo katika kusimamia tatizo la utapiamlo na udumavu katika nchi masikini, kwa muktadha
huo wakiwa Marekani kwenye mkutano wao ndipo alipopata nafasi ya kuongea na ‘Big
win Philanthropy’ ambao walikubali kutoa msaada wa kumsaidia Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika kutekeleza kazi hii ambayo kikosi kazi hiki kimeanza
kuifanya ili kuja na majibu ya kisayansi ambayo atayafanyia kazi”, ameeleza
Bwana Waibe.
Mkurugenzi huyo amesema takwimu za ‘demographic’
za mwaka jana zilizoonesha Tanzana ina udumavu kwa asilimia 30 na takwimu hizo
ndizo zilizoifanya nchi kupata msaada huo
kwa haraka maana nchi ya aina hiyo haiwezi kuendelea kama ina watu
asilimia 30 ambao hawawezi kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.
Ameongeza kuwa changamoto hiyo
ndiyo iliyomsukuma Mhe. Rais kutaka kupata majibu sahihi ya kisayansi ya
visababishi na viashiria vya tatizo hilo nchini ikizingatiwa kuwa mkoa kama
Iringa ambao una vyakula vya kila aina na hali nzuri ya hewa lakini inaongoza
kuwa na udumavu kwa asilimia zaidi ya 50.
“Tatizo hilo sio tuu kwa Iringa
lakini mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini na Mhe. Rais akajiuliza pamoja na
mikataba aliyosaini na wakuu wa mikoa na rasiliamali anazozitoa katika
kupambana na tatizo hili lakini bado haliishi hivyo akaona kuna sababu za
kupata timu ya Watanzania wabobevu ambao watampatia majibu sahihi ili yaweze
kumsaidia kujua ni nini hasa kifanyike ili kumaliza tatizo hilo nchini pale Benki
ya Maendeleo ya Afrika na wadau wengine aliozungumza nao watakapompatia fedha,
ndipo akamua itangazwe tenda watalamu na taasisi mbalimbali ziombe kuifanya
lakini SUA wakashinda kuifanya kazi hiyo ya Mhe. Rais na anayasubiria majibu
kwa hamu sana”, ameeleza Bwana Waibe.
Amewapongeza SUA kwa kushinda
kufanya kazi hiyo kubwa ya nchi na kuwashukuru kwa kukubali ombi la serikali la
kushirikiana na taasisi zingine kwenye kufanya kazi hiyo akiamini kuwa watakuja
na mpango na majibu sahihi ambayo nchi itayatumia katika kutatua changamoto ya
utapiamlo na udumavu nchini.
Kwa upande wake Mtafiti Kiongozi wa
kikosi kazi hicho kutoka Idara ya Sayansi za Chakula na Studi za Walaji (SUA) Prof.
John Msuya amesema utafiti huo utafanyika katika mikoa sita ya Tanzania Bara
ambayo ni Mtwara, Geita, Njombe, Dar es Salaam, Tabora na Iringa na mikoa
miwili ya Tanzania Zanzibar ambayo ni Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.
Mtafiti Kiongozi wa kikosi kazi hicho kutoka Idara ya Sayansi za Chakula na Studi za Walaji (SUA) Prof. John Msuya akieleza kazi ya wataalamu hao. |
Amesema uchaguzi wa mikoa hiyo umezingatia
mabadiliko makubwa ya tatizo hilo yaliyoonekana kwenye taarifa za mwaka 2015 na
2022 ambapo kuna mikoa imefanikiwa kupunguza tatizo katika kipindi hicho na
mingine hali imeongezeka hivyo kuna kitu cha kujifunza kwa mikoa iliyofanikiwa
na ile iliyoshuka.
“Ukiangalia taarifa za mwaka 2015
Mkoa wa Mtwara ulikuwa na udumavu kwa asilimia 38 lakini mwaka 2022 wamepunguza
na kufikia asilimia 22, Kaskazini Pembe kutoka asilimia 34 mwaka 2015 hadi 21
mwka 2022 lakini na ukiangalia Dar es Salaam imepanda udumavu kutoka asilimia
15 mwaka 2015 hadi asilimia 18.40 mwaka 2022, Iringa kutoka asilimia 42 mwaka
2015 hadi asilimia 56.90 mwaka 2022 huku kwa upande wa Zanzibar Kaskazini
Unguja ikipanda kutoka asilimia 23 mwaka 2015 hadi asilimia 29 mwaka 2022”,amefafanua
Prof. Msuya.
Amesema timu hiyo ya watafiti
inakwenda kuangalia mambo makuu mawili ambayo nikutafiti kama matunzo ya watoto
yanaweza kuwa kisababishi cha utapiamlo na udumavu katika mikoa iliyochaguliwa
lakini jambo lingine kubwa ni kutambua na kuchambua mifumo na tabia sababishi
za utapiamlo na udumavu kwenye mikoa hiyo.
Akitoa salamu za Chuo, Naibu Makamu
Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Prof. Amandus Muharwa kwa niaba ya
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha
washirki wote wa zoezi hilo kuwa na mbinu bora na sahihi za ukusanyaji wa
taarifa za kitafiti ili kufikia kusudio la serikali la kuainisha visababishi
vya lishe duni nchini na hatimae kutumia ufahamu huo katika kutengeneza mipango
na mikakati ya kutokomeza tatizo hilo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Prof. Amandus Muharwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda akitoa salamu za Chuo. |
“Mafunzo haya ni muendelezo wa
dhamira njema ya serikali ya kuboresha hali ya lishe chini na kupunguza udumavu
kwa watoto wetu walio chini ya umri wa miaka mitano hali ambayo inarudisha
nyuma afya na maendeleo ya watu wetu”, amesema Prof. Mhairwa.
Naibu huyo wa Makamu Mkuu wa Chuo
Utawala Fedha na Mipango ametumia nafasi hiyo kuihakikishia serikali kama
wasimamizi wakuu wa utafiti huo kuifanya kazi hiyo maalumu ya Kitaifa ya Mhe.
Rais Samia Suluhu Hassan kwa weledi na ubora unaotakiwa ili taifa liweze
kuondokana na tatizo hilo kubwa kwa wananchi wake.
Kikosi Kazi hicho kinajumlisha
wataalamu watano kutoka SUA, mmoja kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara, maafisa
nane waandamizi kutoka Wizara ya Afya, Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Taasisi ya lishe
na Chakula, washiriki wengine nane kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa
wakishirikina na wataalamu na maafisa wa serikali na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Picha ya pamoja ya Mgeni rasmi pamoja na timu ya Wataalamu hao wa Lishe na Chakula wanaounda kikisi kazi hicho cha Kitaifa. |
0 Comments