SUAMEDIA

Ujangili umepungua kwenye maeneo ya hifadhi nchini.

Amina Hezron ,Morogoro.

Matokeo ya utafiti wa mradi wa Biashara, Maendeleo na Mazingira(TRADE Hub) yamebainisha kuwa ujangili kwenye maeneo ya hifadhi umepungua kwa zaidi ya asilimia 58 huku zaidi ya asilimia 83 ya Wananchi wakionekana kupenda Nyamapori kuliko nyama zingine kama vile mbuzi na ngombe.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Charles Mgeni

Hayo yamebainishwa na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Charles Mgeni kupitia wasilisho la utafiti huo wa awali unaotekelezwa na Chuo hicho, uliofanya tathimini ya awali ya urasimishaji wa biashara ya Nyamapori kama inaweza kupunguza ujangili nchini.

Amesema kupitia utafiti huo wamebaini kuwa urasimishaji wa Nyamapori unaweza kupunguza ujangili na kuwa na mchango chanya katika uhifadhi nchini endapo utaratibu,kanuni na miongozo ya usimamiaji biashara hiyo itafuatwa.

Aidha kupitia utafiti huo wametoa angalizo na usimamizi mzuri kwa kuwa kurasimisha kunaweza pia kuongeza ujangili kwa kuwa majangili watawinda na kwenda kuwauzia nyama wenye mabucha ambao wanaweza wasio waaminifu.

Wamezitaka mamlaka za usimamizi kukaa chini na wadau wa nyamapori na kuweka taratibu nzuri ambazo zitawezesha kufanyika kwa biashara hiyo kwa misingi ya haki na kuwa biashara endelevu.

Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na washirika wengine kutoka katika nchi kumi na tano  za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil kuanzia Februari 2019 hadi Machi 2024 ukiangalia biashara ya Soya, Kahawa, Parachichi, Sukari na Wanyamapori.



Post a Comment

0 Comments