SUAMEDIA

SUA yashika nafasi ya tatu MAKISATU

 

Na: Gerald Lwomile

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeshika nafasi ya Tatu upande wa Taasisi za Elimu ya Juu katika Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Ubunifu yaliyofanyika jijini Dodoma kuanzia Aprili 24, 2023 hadi  Aprili 28, 2023.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Prof.Carolyne Nombo alipotembelea banda la SUA kujionea teknolojia na ubunifu mbalimbali

SUA imeshika nafasi hiyo  ikiwa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kikishika nafasi ya kwanza na Chuo Kikuu  Mzumbe  kikishika nafasi ya pili.

Akizungumza katika Kilele cha maonesho hayo hivi karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi ma Teknolojia Prof. Adolf F. Mkenda (MB) amesema, serikali itahakikisha inaendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama Ibara ya 102 ya Ilani ya CCM inavyosema

Amesema Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni mambo yanayoweza kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa haraka kama ambavyo hivi sasa kuna Kampuni ya TANZTECH ambayo itaanza  kuzalisha vishikwambi nchini

Waziri wa Elimu, Sayansi ma Teknolojia Prof. Adolf F. Mkenda (MB) alipotembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya MAKISATU

Prof. Mkenda amesema endapo mpango huo utaanza basi wataungana na Serikali kupitia vyuo mbalimbali ili kusaidia wanafunzi kuwa na mafunzo maalum ya masuala ya kielektroniki na uhandisi.

Akizunguma katika kilele cha maonesho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Prof.Carolyne Nombo, amesema tangu kuanzishwa kwa Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ya mwaka 2019, wabunifu na wavumbuzi wachanga zaidi ya 2,600 waliibuliwa na kutambuliwa Wizarani  hapo.

Amesema maonesho hayo ni mkakati wa serikali ya awamu ya sita  kuhakikisha kunaibuliwa teknolojia na bunifu mbalimbali  ili kuhakikisha taifa linapiga hatua katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema serikali imechukua hatua za kuhakikisha inawaendeleza wabunifu 283 kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili ubunifu wao ukamilike na kuingizwa sokoni.




Post a Comment

0 Comments