Na: Tatyana Celestine
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kukiwezesha chuo hicho kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi yaani (Higher Education for Economic Transformation [HEET] ambapo SUA imetekeleza adhma ya mradi huo kwa kupeleka wafanyakazi masomoni, kuongeza ujuzi, kununua vifaa vya kufundishia pamoja na Ujenzi wa Miundombinu chuoni hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda. (Picha Maktaba) |
Prof. Chibunda amesema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi katika Maadhisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani ambapo amesema Wafanyakazi wa Chuo hicho wanaendelea kunufaika moja kwa moja na fedha za Mradi wa HEET kiasi cha Sh. bilioni 73 ambazo pamoja na matumizi mengine pia zitawezesha kuboresha upande wa TEHAMA ambao Chuo hicho hakitakuwa na changamoto ya mtandao hivyo kusaidia utendaji kazi bora sambamba na ukuaji wa Teknolojia duaniani katika ufundishaji kwa njia ya mtandao.
Aidha Prof. Chibunda amepongeza namna wafanyakazi wote bila kujali vyama vyao walivyoweza kuonesha mshikamano na kushirikiana hali ambayo imechangiwa na kuwepo kwa Mwongozo mpya wa Uchaguzi wa Wafanyakazi Bora ulioanza kutumika mwaka huu na hivyo kuwataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi vilivyopo SUA yaani RAAWU na THTU kuzichukua na kuzifanyia kazi changamoto zilizooneka katika mwongozo huo ili kuuboesha zaidi.
Akizungumzia kuhusu stahiki za wafanyakazi Makamu huyo wa Mkuu wa Chuo cha SUA amesema Serikali imetoa muongozo katika uboreshaji stahiki za wafanyakazi nchini na kwamba Chuo cha SUA kimekuwa moja ya Taasisi ambazo zimekwisha anza utekelezaji kwa wafanyakazi wake kwa kuanza kulipa madeni ya wafanyakazi , kutoa stahiki kikamilifu kwa wastaafu , kuwalipa wafanyakazi fedha za likizo kutokana na hilo ametoa agizo kwa Wakuu wote wa Idara, Ndaki, Kurugenzi na Shule Kuu kuhakikisha wanatoa ruhusa ya likizo kwa wafanyakazi kwani likizo ni haki ya kila mfanyakazi.
Pia amewataka Viongozi kuwaruhusu wafanyakazi wote kujitokeza kushiriki katika michezo mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kushiriki mashindano ya ndani na nje ya Chuo na kuahidi kuwa kuanzia sasa SUA itashiriki shughuli za Mei Mosi ikiwemo michezo kila mwaka popote zitakapofanyika nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi RAAWU SUA Bw. Faraja Kamendu ameipongeza Menejimenti ya Chuo kwa namna inavyowajali wafanyakazi wake kwa kushughulikia madai mbalimbali ya wafanyakazi hao na kuiomba Menejimenti hiyo kuendelea kushughulikia Stahiki za waliokuwa wafanyakazi wenye vyeti visivyo na sifa ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Chibunda amemuhakikishia kuyafanyia kazi kikamilifu kulingana na muongozo husika katika kila jambo.
Nae Dkt.Justine Maganira kutoka Idara ya Sayansi za Viumbe Hai ambaye ni Mfanyakazi Bora namba moja wa SUA kwa mwaka 2023 amewataka wafanyakazi kuongeza juhudi katika kazi pamoja na ushirikiano na wengine kwani ndio siri ya ushindi wa Tuzo hiyo kwa kuwa SUA ina wafanyakazi walio bora, wanaojituma na waadilifu hivyo anategemea miaka ijayo mshindi kitaifa atatoka SUA .
Akielezea sababu ya kushika nafasi ya ushindi wa pili wa Chuo Mfanyakazi Bora 2023 chuoni hapo Bi. Vaileth Bupamba ameshukuru Chuo kwa kumuamini na kuona jitihada zake katika kazi na kusema kuwa zawadi hiyo ni chachu kwake katika kufanya vizuri zaidi miaka ijayo.
Jumla ya wafanyakazi 74 wamepata zawadi ya wafanyakazi bora ambapo Dkt. Justine Maganira kutoka Idara ya Sayansi za Viumbe Hai amekuwa mfanyakazi Bora wa Chuo namba moja kufuatiwa na Bi Vaileth Bupamba kutoka Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo, Sherehe hizo za Mei Mosi 2023 zimebeba kauli mbiu isemayo “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi” Wakati ni sasa.
KATIKA PICHA BAADHI YA WAFANYAKAZI BORA WAKIPOKEA ZAWADI ZAO KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MEI MOSI KUPITIA CHUO KIKUU CHA SOKOINE CHA KILIMO (SUA)
0 Comments