SUAMEDIA

Serikali isome akili za vijana kabla ya kuwasukuma kwenye kilimo waingie kwa kukipenda sio kulazimishwa

 

Na: Winfrida Nicolaus

Vijana nchini Tanzania wametakiwa kuingia kwenye shughuli za Kilimo kwa kukipenda na sio kulazimishwa au kukifanya cha ziada kwa kuwa ili ufanikiwe kwenye jambo lazima ulipende ili ufanye kwa moyo wote na kupa tija.

Waziri Mstaafu wa Kilimo wa Serikali ya awamu ya kwanza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukizi ya Mwl. Nyerere Mzee Paul Kimiti akiongea kwenye maadhimisho hayo kama mchokoza mada.

Hayo yamebainishwa na aliyekuwa Waziri Mstaafu wa Kilimo wa Serikali ya awamu ya kwanza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukizi ya Mwl. Nyerere Mzee Paul Kimiti wakati akiongoza Majadiliano kuhusu Historia za Vijana na fursa za kilimo Tanzania kwenye Maadhimisho ya Kumbukizi ya 18 ya Hayati Edward Moringe Sokoine yaliyofanyika viwanja vya Michezo vya Kampasi Kuu ya Edward Moringe ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Mkoani Morogoro

Hapo zamani walikuwa na utaratibu kuwa ukiwa shule ya (Middle School) kazi za Kilimo zilikuwa ni za kawaida kwa maana ya unajifunza kilimo na baada ya muda unakipenda hivyo hulazimishwi kuingia kwenye kilimo, lazima ukipende ambapo vijana wanatakiwa kupewa utaalam ikiwezekana waingie kwenye kilimo lakini jambo la msingi kwao ni kukipenda kwanza”, alifafanua Mzee Kimiti.

Aidha amesema jitihada ya Serikali pamoja na Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Nyerere alitaka kuhakikisha vijana wanajishughulisha katika mambo ya kilimo ndio maana kukaanzishwa Mfuko wa Rais wa kujitegemea ambao Baba  wa Taifa mwenyewe aliandika utangulizi akisema madhumuni ya Mfuko huo ni kujaribu kubadilisha fikra na msimamo wa vijana kuhusiana na kilimo.

Amesema kupitia Mfuko huo Baba wa Taifa aliitaji kila mtu achangie kulingana na uwezo wake na hapo Mchango wa Hayati Sokoine ulionekana kwani alikubali na kuamua kutoa nusu ya mshahara wake kukatwa kila mwezi ili kuchangia Mfuko huo lengo ni kuhakikisha vijana wanajishughulisha na Kilimo na kila mtu anafanya  kazi.

“Sokoine aliniambia Kimiti wewe ni Mtaalam wa kilimo hawa vijana wanakaa tu tunafanya Nini?, nikamjibu Mimi nimeshaanza kuandika vitabu, akasema sasa vitabu hivyo tutaweka sheria na sheria yenyewe ikasema kila mtu afanye kazi hapo tunaona jinsi gani Serikali yenu ya awamu ya kwanza ilivyokuwa ikijitahidi na sisi kama waasisi wa nchi hii tuliobaki tunataka vijana tuwarithishe wajue jitihada tunazofanya kwanzia mwanzo mpaka mwisho”, alisema Paul Kimiti

Aidha Bwa. Kimiti amesema Hayati Sokoine alikuwa kati ya viongozi wenye msimamo wa kipekee, kiongozi aliyekubali kuacha Familia yake yote na kujitolea ya kuwa kila kiongozi yupo mahali alipo kwaajili ya watu na cheo ni dhamana tu watu ndio wamewafikisha mahali walipo na hayo walikuja kuyatambua wakati amefariki yeye alietaka kila siku kuwasaidia watanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Jaji Joseph Sinde Warioba amesema wao walizaliwa kipindi ambacho kilimo kilikuwa ni kazi na ndio utamaduni lakini wakati kwa sasa zinatafutwa njia ya kuwafanya vijana waende kufanya kazi.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Jaji Joseph Sinde Warioba akichangia mada kwenye Mdahalo huo.

Amesema imefika mahali kilimo kimekuwa sio kazi hivyo ni muhimu zitengenezwe Sera na Miongozo ambayo itawafanya vijana wapende Kilimo na ili kukamilisha hillo lazima kuingia kwenye fikra zao.

 “Kama unakwenda kwenye kilimo upende kilimo kama haupendi hata ukitengenezewa BBT haitakusaidia kitu hivyo jambo muhimu ni kuelewa mawazo ya vijana ili kutengeneza Sera zitakazowafanya vijana hao kuingia kwenye kilimo zaidi kwa kuanza na wale wanaopenda kilimo”, alieleza Jaji Warioba

Amesema Kilimo bado kitabaki kuwa msingi wa maisha ya kila mmoja kwa kuwa kujitegemea kunategemea kilimo hivyo mchango wake kwenye pato la Taifa unatakiwa kuwa mkubwa zaidi ndio maana ni muhimu kuwa na Sera ambazo zitafanya Kilimo kuwa msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi.

PICHA ZA WASHIRIKI WA MDAHALO HUO WAKIFUATILIA MJADALA.







Post a Comment

0 Comments