Na: Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo kama kilivyopewa
dhamana ya kutunza jina la Hayati Edward Moringe Sokoine ikiwa ni alama ya
kudumu ya kiongozi huyo shupavu na mahiri kimetakiwa kuendeleza jitihada za
kukuza Sekta ya Kilimo nchini kwa kuendelea kufanya Tafiti kwa nguvu zote na
kutoa mafunzo stahiki kama sehemu ya kuenzi mchango wa Sokoine.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Ngulu akizungumza kwenye Mdahalo wa kumbukizi ya Hayati Sokoine. |
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya
Mvomero Mhe. Judith Ngulu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Mdahalo
wa Kitaifa wa Maadhimisho ya Kumbukizi ya 18 ya Hayati Edward Moringe Sokoine
na hitimisho la Maadhimisho hayo ambayo yaliyoanza Mei 23, 2023 katika Kampasi
Kuu ya Edward Moringe Mkoani Morogoro.
Amesema wanapokutana katika
Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe wasiishie tu kusherehekea maisha yake ya
kuvutia bali waweke nadhiri ya kuendeleza maono yake na kuiga matendo mazuri
ikiwa ni pamoja na namna alivyojitoa kuwatumikia watanzania na kuwaletea
maendeleo kwa kipindi cha uhai wake kwakuwa alihimiza kwa kiasi kikubwa mabadiliko
katika nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, elimu, viwanda pamoja na sekta
zingine.
Aidha amesema anatambua kuwa
uanzishwaji wa (SUA) ni sehemu ya matunda ya Hayati Sokoine na maono yake pia na
matokeo ya utendaji kazi wake yanaonekana hivyo (SUA) inatambulika kama Chuo
mama ambacho kimekuwa kikitoa mchango mkubwa kwa Serikali na hata Taifa katika
maswala ya tafiti, kutoa mafunzo, ubunifu wa vitu mbalimbali kwani hayo ni
matokeo ya matunda ambayo Hayati Sokoine ameyaacha.
“Hayati Sokoine alisisitiza
kujitosheleza kwa chakula, ninamnukuu alisema “Wajibu wa kila Mtanzania kila
familia na anayekula na kujilisha yeye mwenyewe si wajibu wa Taifa kumlisha
mtu, unaweza ukasaidiwa unapopatikana na janga lakini kama hauna janga ni
wajibu wa kila mtu aweze kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa Taifa
kauli hii aliitoa octoba 4, 1983”, alisema Mhek Nguli
Mhe. Judith ameongeza kwa
kuwaambia vijana kuwa wamepewa fursa na Serikali imeweka nguvu kubwa kwao hivyo
wanatakiwa kuachana na ujana ambao umepitiliza utakaowasababisha kushindwa
kutimiza malengo yao na kukumbuka kuwa kuna maisha baada ya ujana.
Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa
Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema wanafanya mihadhara
ya Kumbukizi ya Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa vipindi viwili
tofauti mwaka 1977 – 1980 na 1983 – 1984 kutokana na ushiriki wake mkubwa
katika harakati za kuanzishwa kwa Chuo hicho vilevile kutambua mchango wake
katika maendeleo ya nchi.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda akieleza malengo ya SUA kufanya kumbukizi hiyo. |
Amesema
tangu kuanzishwa kwa kumbukizi hizo mada mbalimbali kuhusiana na maswala kama
vile mfumo wa Vyama vingi, Demokrasia, Rushwa, Kupambana na Umasikini, Tanzania
baada ya Nyerere, Usalama wa Chakula, Maendeleo ya Kilimo, Elimu, Utafiti, Utatuzi
wa Migogoro, Utandawazi na mambo mengine yanayohusiana na maswala ya Kijamii,
Kisiasa na Kiuchumi yamejadiliwa.
Prof.
Chibunda ameongeza kuwa Kauli Mbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha vijana
kushiriki kikamilifu katika Sekta ya ilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuweka
Mazingira rafiki, Sera na Miongozo inayowawezesha kufanya shughuli za kilimo, ufugaji
na Uvuvi kwa ufanisi.
‘‘Kauli
mbiu hii inaumuhimu mkubwa katika kuendeleza kazi na ndoto za Hayati Edward
Moringe Sokoine na kuwapa vijana matumaini na muongozo wa kufanikiwa katika
Sekta hizi muhimu”, amesisitiza Prof. Chibunda.
Wageni mbalimbali wakifuatilia mdahalo huo wa 18 wa kumbukizi ya Hayati Sokoine uliofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe Mkoani Morogoro. |
0 Comments