Na: Amina Hezron, Morogoro.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya Tani elfu mbili za Nyamapori inayowindwa kiharamu kupitia ujangili kwenye maeneo yaliyohifadhiwa yenye thamani ya dollar za Kimarekani milioni 50 hukamatwa kila mwaka nchini na hivyo kukwamisha juhudi za uhifadhi wa Wanyama hao.
Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Charles Mgeni kupitia wasilisho la utafiti wa awali wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub). |
Hayo yamebainishwa na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Charles Mgeni kupitia wasilisho la utafiti wa awali wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) unaotekelezwa na Chuo hicho, uliofanya Tathimini ya awali ya urasimishaji wa biashara ya Nyamapori kama inaweza kupunguza ujangili nchini.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa biashara hiyo ya Nyamapori haiishii ndani ya Tanzania na Afrika pekee bali huvuka hata mipaka ya Afrika na hii ni baada ya kuripotiwa kukamatwa kwa nyama hiyo kwenye mabegi nchini Ufaransa kwenye uwanja wa ndege ikionesha kuwa ainatoka Afrika.
“Katika swala hili Waataaluma wamegawanyika katika makundi mawili katika mawazo ya kitafiti ya namna ya kumaliza tatizo la ujangili ambapo kundi la kwanza linapendekeza kuweka sheria kali za kuzuia uuzwaji wa Nyamapori na bidhaa zake huku kundi la pili wakipendekeza urasimishwaji wa biashara hiyo ili kuzuia ujangili”, alieleza Dkt. Mgeni.
Moja ya Bucha rasmi za uuzaji wa nyamapori lililosajiliwa na kupewa vibali Jijini Arusha. |
Akifafanua Mawazo ya kundi la kwanza amesema kuwa linaona uzuiaji wa biashara hiyo kwa kuweka sheria ngumu na kali utasaidia kupunguza ujangili na hasa ikizingatiwa kuwa nyama hiyo isiyopimwa na kuangaliwa vizuri inaweza kusababisha athari za kiafaya kwa watumiaji kutokana na magonjwa mengi ya Wanyama huambukiza binadamu kama vile Ebola, HIV,Uviko na mengine.
Aidha amesema kundi la pili la Wanazuoni linalopendekeza kurasimisha lionana biashara hiyo itakuwa tiba ya tatizo la ujangili kwakuwa Wananchi hawatakuwa na sababu ya kwenda kufanya ujangili kwani Nyamapori itapatikana kwenye mabucha kihalali kupitia uvunaji endelevu na hivyo jamii itaona faida ya kutunza maliasili hiyo kwa kupata kipato na chakula.
Mtafiti huyo amesema pamoja na kuwa na makundi hayo mawili lakini Wanazuoni wengi wanapendekeza njia ya pili ya urasimishaji wa biashara ya Nyamapori inaweza kuwa muafaka kwani jamii itajiona ina wajibu wa kutunza maliasili kwakuwa wanafaidi matunda ya Wanyama hao kwa kuwapa kipato, Ajira na mboga katika maeneo ambayo yanazunguka hifadhi.
Amesema mapendekezo hayo ya wanazuoni wengi pengine ndiyo yalimsukuma Rais wa awamu ya tano Marehemu John Pombe Magufuli kutangaza urasimishaji huo na uanzishwaji wa mabucha ya Nyamapori na kuitaka Wizara na taasisi za usimamzizi kuweka miongozo ya ufanyikaji wa biashara hiyo hapa nchini.
Dkt. Mgeni amesema kupitia mradi huo wa TRADE Hub wameona wafanye tathimini ya kina kuangalia namna biashara hivyo inavyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini lakini pia kuangalia taratibu,kanuni na mifumo ya uendeshaji wa biashara hiyo ilivyowekwa ili ifanyike vizuri kwa kukutana na wadau wote katika ngazi na mamlaka mbalimbali.
Mradi wa Utafiti wa
Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano
unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana
Taasisi zingine zaidi ya 50 duniani na kutoka katika nchi 15 za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil na
kufadhiliwa na Mfuko wa Utafiti wa Changamoto za Kidunia wa Serikali ya
Uingereza (UKGCRF) na Mfuko wa Pamoja wa Utafiti na Ubunifu (UKRI).
Picha kwa hisani ya http://tembeatz.blogspot.com |
0 Comments