Na: Amina Hezron, Kilimanjaro.
Imebainika kuwa kanuni, Sera, Masharti na vigezo
vinavyowekwa kwenye Soko la dunia na wanunuzi wengine hususani nchi za Ulaya
ndio sababu kuu ya Mazao mengi ya wakulima nchini kutosafirishwa kuuzwa nje na
kupata faida kubwa.
Prof. Reuben Kadigi ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) akizungumza mbele ya wadau wa mradi huo Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro. |
Hayo yamebainishwa kwenye warsha ya wadau na Prof. Reuben Kadigi ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) wakati akieleza matokeo ya jumla ya Mradi huo unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine ha Kilimo (SUA) nchini Tanzania na kwenye nchi zingine 15 za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil.
“Wahitaji wanunuzi wa
bidhaa zetu wanaenda wanabadirika wakiweka vigezo kanuni na sheria
mbalimbali zinazotakiwa kuzingatiwa wakati wa uzalishaji ikiwemo uzalishaji
unaolinda mazingira, haki kwa wafanyakazi kwenye kuzalisha zao hilo na mengine
mengi ambayo ukiangalia kwa nchi yetu na nchi nyingi zinazoendelea hiyo inakuwa
kikwazo kikubwa hivyo lazima nchi yetu tujipange kutimiza vigezo hivyo ili
tunufaike”,alieleza Prof. Kadigi.
Aidha amesema kufuatia changamoto hiyo nchi nyingi
zinashindwa kufikia vigezo hivyo na kupelekea pale wanapokwenda kuuza kwenye
mataifa hayo mazao na bidhaa zao zinakuwa na ushindani mkubwa kwakuwa kuna watu
wanaojitangaza zaidi huko na wameweza kukidhi viwango hivyo vinavyotakiwa na
soko.
Mtafiti huyo Mkuu wa Mradi wa TRADE HUB amesema jitihada za
pamoja zinatakiwa kati ya
Serikali,Wakulima na Makampuni makubwa ambayo yanasafirisha Mazao nje ya nchi
kuwakingia mgongo wakulima wa Tanzania kwa kuwasaidia kufikia vigezo kwakuwa
ili kutambuliwa pia kuna gharama kubwa ambazo wakulima wadogo na vyama vya
ushirika haviwezi kumudu.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka Programu ya
Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) katika kituo cha Dunia cha Ufatiliaji wa
Uhifadhi (WCMC) Prof. Neil Burgess amesema mradi huo unafanya utafiti kuangalia
Biashara, Maendeleo na Mazingira ya mazao ya Kilimo na Wanyamapori katika nchi
washiriki.
Prof. Neil Burgess Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) katika kituo cha Dunia cha Ufatiliaji wa Uhifadhi. |
“Huu ni mradi wa utafiti wa kimataifa unaoangalia sera za
kimataifa za biashara, Usimamizi wa bishara na Kanuni za biashara lakini pia
faida na hasara za kanuni zilizowekwa kimataifa kwenye biashara mfano mzuri ni
hizi za Umoja wa Ulaya ambazo zinaonekana kuathiri nchi nyingi zinazoendelea”,
alifafanua Prof. Burgess.
Amesema kazi field na kukusanya taarifa zimemalizika
na sasa wameweka nguvu katika kuandika matokeo kwa kufanya utambuzi wa kina ili
kupata kitu ambacho kitakuwa na faida kutumika kwa taifa, Watunga sera na
Wakulima ambao wanaguswa na mifumo mbalimbali ya uzalishaji.
Mradi wa Utafiti wa
Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano
unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana
Taasisi zingine zaidi ya 50 duniani na kutoka katika nchi 15 za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil na
kufadhiliwa na Mfuko wa Utafiti wa Changamoto za Kidunia wa Serikali ya
Uingereza (UKGCRF) na Mfuko wa Pamoja wa Utafiti na Ubunifu (UKRI).
Wadau wakifuatilia mawasilisho na matokeo ya utafiti huo. |
0 Comments