SUAMEDIA

SUA yazindua Kamati ya Ushauri wa Viwanda katika kukuza na kuinua uchumi kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Na: Tatyana Celestine

Katika kutekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi yaani (Higher Education for Economic Transformation [HEET] project) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia Chuo Kikuu cha Sokine cha Kilimo (SUA) wamezindua Kamati ya Ushauri wa Viwanda leo Aprili 29 ili kushirikiana na Serikali katika kukuza na kuinua uchumi nchini Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

 

Akizungumza na watekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wakati wa Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Viwanda mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu ya Juu Prof. James Mdoe akimuwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf  F. Mkenda amesema kuwa zoezi hilo ni moja ya utekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2020 -2025 kuufikisha mradi huo kukamilika kwa ubora na wakati ili kuboresha Elimu ya Juu.

Aidha amesema kuwa hapo awali hapakuwa na mfumo rasmi kwa Vyuo Vikuu kuwezesha kukaa pamoja na kuchakata mahitaji muhimu ili kufanikisha Elimu Bora pia ajira imepelekea kuwa na ombwe na sasa imekuwa rasmi Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kama moja ya wanufaika na mradi wa HEET kamati hiyo ikasaidie kutoa wanafunzi wenye taaluma na wanaohitajika katika ulimwengu wa kazi na kufikia malengo ya viongozi wao nchini.

Naye Muwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bw. Kaboko Mkalinga amewataka waajiri kujitoa vyema katika utekelezaji wa mradi huo kutokana na uzoefu walionao hivyo wahakikishe wanatoa mchango wao kwa wananchi na kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kwa kutengeneza uzalishaji wa ajira nchini.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Viwanda nchini Tanzania Bw. Akida Mnyenyelwa amesema kamati iliyochaguliwa ni muhimu kwa lengo la kuleta maendeleo ya viwanda hivyo kamati hiyo iliyoundwa ikatekeleze majukumu yake ikizingatia sekta hiyo na umuhimu wa viwanda nchini.

Aidha Bw. Mnyenyelwa amevitaka Vyuo kuwa na ushirikiano na viwanda ili waweze kujua  viwanda vinavyoendeshwa ili iwasaidie kutengeneza mitaala yenye kuleta tija kwa kutambua fani na ujuzi unaohitajika kwenye viwanda pia  tafiti zitakazofanywa zinazohusu viwanda kutoka SUA na Vyuo vingine nchini wahakikishe wanaleta mrejesho kwa wamiliki wa viwanda ili kutambua changamoto na wapi pa kufanyia kazi.

Akizungumzia majukumu ya wajumbe wa kamati iliyozinduliwa Kiongozi wa Mradi wa HEET kwa upande wa  uhusiano na Taasisi binafsi Dkt. Felix  Nandonde kutoka SUA amesema kuna majukumu 11 katika utekelezaji wa mradi huo lakini ameyataja majukumu manne ambayo yanayowalenga moja kwa moja ni pamoja na kubuni na kutekeleza mipango bora katika kutengeneza ajira, kushauri Chuo katika kubuni mitaala bora yenye uhitaji,kutafuta nafasi za mafunzo kwa vitendo ya muda mrefu kwa wanafunzi na waadhiri, kushawishi sekta binafsi kuweka fedha katika tafiti za Chuo.

 Awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET)  Prof. Amandus Mhairwa amesema kuwa SUA imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 73.6 ambazo ni sawa na Dola za kimarekani Millioni 32  zilizogawanywa kutumika katika makundi mawili ambayo Bilioni 55.2 zitatumika Kampasi Kuu ya Edward Moringe na kiasi cha shilingi Bilioni 18.4 kitatumika Kampasi  ya Katavi kwa lengo la kuboresha elimu kwa Chuo hicho.

 
















KATIKA VIDEO FUATILIA UZINDUZI KAMATI YA USHAURI WA VIWANDA 

 

Post a Comment

0 Comments