SUAMEDIA

SUA na Chuo Kikuu cha Copenhagen kujipanga kutatua changamoto za chumvi ardhini

Na: Hadija Zahoro

Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo ( SUA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Copenhagen cha nchini Denmark,  kimejipanga kutatua changamoto za chumvi ardhini  pamoja na mafuriko zinazoathiri uzalishaji wa zao la mpunga kupitia mradi wa ‘Climate Smart African Rice Research Project’ unaolenga kuzalisha aina ya mpunga ambao unaweza kuvumilia changamoto hizo.

Akizungumza na SUAMEDIA Prof. Susan Nchimbi  Msolla, kutoka Idara ya Mimea Vipando  na Mazao ya Bustani,amesema  kuwa wakulima wengi  hasa wanaopanda mbegu  moja kwa moja bila kupandikiza vishina, wanakumbana na adha ya mazao kung’oka, kusombwa na mafuriko na tatizo la chumvi katika sehemu nyingi zinazolimwa zao hilo hasa katika skimu za umwagiliaji.

‘‘Kuna huu mradi ambao umeanza tangu 2020, tuna wanafunzi   kama saba hivi, wa 3 kutoka shahada ya uzamivu  na wengine waliobaki  wanafanya uzamili na lengo kubwa  ni kuweza kuzalisha mpunga  hata kwenye maeneo ambayo yameathirika. Anaeleza Prof. Susan

Kwa upande wake Prof. Ole Pedersen  kutoka  Chuo Kikuu cha Copenhagen cha nchini Denmark ambaye pia ndiyo mwanzilishi wa mradi huo, amesema kuwa wamechagua SUA kuwa mshiriki wao wa kwanza  kutokana na historia ndefu waliyojenga kati ya SUA na DANIDA.

‘‘Lengo kubwa ni kuandaa uzalishaji mpya wa mpunga utakaoendana na  hali ya maeneo mbalimbali  Afrika  kutokana na kuathiriwa na chumvi pamoja na mafuriko ambapo  tunaweza kuendeleza uzalishaji bora  wa mpunga  hasa Tanzania na matarajio yangu kwa miaka miwili na nusu au  miaka mitatu ijayo kutoka sasa  kutakuwa na wakulima wapya kutoka Copenhagen  ambao watakuwa tayari kuja Tanzani pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki ili kusaidia. Anabainisha Prof. Ole

Nae, Mtafiti kutoka TARI Dkt. Atugonza Bilaro, amewaasa wakulima kutoa taarifa haraka kwa wataalamu kwani wao kama watafiti wanafanya tafiti ambazo zinakuja na majibu ambayo yanawahusu wao na kwa kufanya hivyo itasaidia kufanya uzalishaji wenye tija.

 

Mradi huo pia unashirikiana na  taasisi nyingine ikiwemo Taasisi ya kimataifa ya Utafiti wa Mpunga ya nchini Ufilipino (IRRI), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja  na Wakala wa Taifa wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mbegu za Kilimo (ASA) pamoja na kudhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Denmark(DANIDA).

 

 








 






 

 

 

Post a Comment

0 Comments