Na: Calvin Gwabara
– Morogoro.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Maziwa Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wao Prof. Zacharia Samweli Masanyiwa wamefanya ziara ya kimafunzo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kuzungunza na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Tihelwa Chibunda kabla ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Chuo hicho.
Picha ya pamoja ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda na Wajumbe wa Ushauri wa Bodi ya Maziwa Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Zacharia Samweli Masanyiwa.
Akieleza malengo ya ziara hiyo Chuoni hapo mara baada ya mazungumzo na Prof. Chibunda, Mwenyekiti wa bodi hiyo Prof. Zacharia Samweli Masanyiwa amesema wamefika sehemu sahihi ya kujifunza kwakuwa Chuo hicho ndicho kinachozalisha wataalamu wa mifugo nchini.
“Tunafahamu
kuwa tasnia ya maziwa ni sehemu ya Sekta kubwa ya Mifugo nchini hivyo tumekuja
kuona na kujifunza wanafanya nini lakini wameona kuwa SUA ndio wadau wakubwa wa
Mifugo kwakuwa wanafundisha wataalamu wetu na wana mashamba ya mfano ya mifugo
ili kuzalisha maziwa mengi” alisema Prof. Masanyiwa.
Kwa upande
wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda
amewaambia wajumbe hao wa Bodi ya Ushauri ya Maziwa nchini kuwa Chuo kipo
kwenye mkakati mkubwa wa maboresho wa shamba la mifugo na uzalishaji wa maziwa.
Amesema kwa
sasa wanacho kitengo kidogo cha usindikaji maziwa lakini kupitia Mradi wa
Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wamepata fedha za kujenga kiwanda
kikubwa cha Usindikaji wa maziwa na kuboresha shamba lake.
Bodi ya
Maziwa imeundwa kwa Sheria ya Tasnia ya Maziwa Sura (262) ambayo iko chini ya
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yenye jukumu la kusimamia, kuratibu na
kuendeleza tasnia ya maziwa.
Bodi ya Maziwa
inajukumu la kuhamasisha na kuwawezesha wadau katika shughuli za uzalishaji,
ukusanyaji maziwa, usindikaji, kuboresha masoko na unywaji wa maziwa na bidhaa
zake.
Lengo kuu la
bodi hiyo ni Kuwa na tasnia ya maziwa inayosimamiwa na kuratibiwa vizuri, yenye
ushindani kwa lengo la kuboresha maisha ya watanzania na kuongeza mchango wa
tasnia ya maziwa katika uchumi wa Taifa.
Kazi za Bodi ya Maziwa zimeelezwa katika Sheria ya Maziwa ya mwaka 2004 (Sura ya 262) ibara ya 10 kuwa ni:Usimamizi wa shughuli zote zinazofanywa katika tasnia ya maziwa, Kuendeleza tasnia ya maziwa kama vile kufanya promosheni za unywaji maziwa, Kushawishi uanzishaji wa programu za unywaji maziwa shuleni, Kutoa mafunzo kwa wadau wa maziwa, kusajili wadau, Kuibadilisha sekta ya maziwa isiyo rasmi kwenda kwenye sekta rasmi, Kuboresha mazingira ya biashara katika tasnia ya maziwa na Kuratibu wadau wa tasnia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Maziwa Tanzania Prof. Zacharia Samweli Masanyiwa akizungumza na SUAMEDIA nje ya kikao hicho.
0 Comments