Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Tafiti zimeonesha kuwa, kwa mwaka mmoja Tanzania inapoteza
zaidi ya shilingi bilioni 19 kutokana na athari zinazotokana na Minyoo tegu ya
Nguruwe kwa jamii ikiwemo matibabu na kutupa nyama yenye maambukizi.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Kisayansi CYSTINET Africa Prof. Helena Ngowi akiwasilisha matokeo ya utafiti kwenye warsha hiyo jijini Dodoma. |
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mtandao wa Kisayansi
CYSTINET Africa Prof. Helena Ngowi kwenye Warsha ya kujadili
mrejesho wa matokeo ya Utafiti kuhusu namna
ya kudhibiti Mnyoo Tegu ya Nguruwe Tanzania iliyofanyika Jijini Dodoma.
“Ukiangalia hapa nchini Tanzania wagonjwa wa kifafa
takribani 212 ya wagonjwa wote wa ugonjwa huo utakuta wanatokana na Minyoo tegu
ya Nguruwe na kuigharimu jamii shilingi bilioni 12 kwaajili ya matibabu na hasara
ya shilingi bilioni 7 kutokana na kutupwa kwa nyama ya nguruwe nyenye
maambukizi, alifafanua Prof. Helena.
Aidha Prof. Helena amesema pamoja na magonjwa
yanayosababishwa na tegu wa Nguruwe (Taenia solium) kuwa na athari
kiuchumi,kiafya na kijamii kwa waathirika na familia zao lakini hayajapewa
kipaumbele nchini Tanzania.
Mkurugenzi huyo wa CYSTINET Afrika amesema kimataifa,kwa
mujibu wa ripoti yam waka 2014 ya
Shirika la Chakula duniani FAO na Shirika la afya Duniani WHO mnyoo tegu wa nguruwe ni tishio namba moja kati
ya magonjwa ya vimelea kundi hili yanayoenezwa kwa njia ya chakula.
“Muhtasari huu wa matokeo umetokana na uchambuzi wa
kina wa matokeo ya tafiti yaliyochapishwa katika kipindi cha miaka 26 hadi
kufikia Disemba 2021 Tafiti
hizi zilifadhiliwa na wafadhili mbalimbali, ikiwemo Serikali ya Tanzania (hasa
kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi)” alieleza Prof. Ngowi.
Hata hivyo amesema Tafiti zaidi zinahitajika kubaini
ukubwa wa tatizo na kutafuta suluhisho endelevu ingawa tayari katika kipindi
cha mwaka 1995 -2021 zimefanyika tafiti zaidi ya 78 zikiwemo zilizohusu kiwango
cha mambukizi kwa binadamu, kiwango cha maambukizi kwa nguruwe, mgongano wa
magonjwa mengine, vichocheo vya maambukizi, madhara ya kiuchumi, kudhibiti
maambukizi kwa binadamu, kudhibiti maambukizi kwa nguruwe, Mikakati ya elimu
kwa jamii pamoja na Nyanja zingine ndogo ndogo,
Prof. Helena amesema tafiti nyingi zinaonesha
zililenga kuangalia maambukizi kwa nguruwe na matokeo mengi ya tafiti hizo
yameonesha maambukizi kwa nguruwe waliopo vijijini waliochunguzwa kwa kukagua kwenye
ulimi maambukizi ni asilimia 6.0% – 17.4% na kwa kipimo cha Ag-ELISA ni 1.5% – 33.3%.
Amesema matokeo ya utafiti ya Mnyoo kamili tumboni kwa
binadamu (taeniasis) kwa kipimo cha Coproantigen
ELISA ilionesha ni 2.3% – 5.2%, utafiti wa vimelea mwilini mwa binadamu
(cysticercosis) kwa kipimo cha Antigen
ELISA imeonesha ni 16.7%, Vimelea kwenye ubongo wa binadamu
(neurocysticercosis) vipo kwa wagonjwa wa kifafa zaidi wakati Vimelea kwenye
nyama ya nguruwe kwa ukaguzi wa kaiwaida wamebaini ni asilimia 0% - 18.2%.
Mtafiti huyo kutoka SUA amesema
vichocheo vikubwa vya maambukizi hayo ya Minyoo tegu ya nguruwe ni Ufugaji wa
nguruwe wa kienyeji wa kuacha kuzagaa mitaani kujitafutia chakula lakini pia
kutokuwepo kwa vyoo kwenye maeneo yanayofuiga nguruwe kwa wingi hasa vijijini
bila kusahau kutopika nyama hiyo vizuri.
Kwa upande wake Dkt. Benard James
Ngowi ambaye ni Mtafiti na Mhadiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam kutoka
Ndaki ya afya na sayansi shirikishi kampasi ya Mbeya na Mtafiti mwandamizi
katika taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu kituo cha NIMR Muhimbili
amesema matokeo yanaonekana kwa binadamu katika hali mbili ambapo ya kwanza ni
ile ya binadamu anakuwa na mnyoo kamili kwenye utumbo na ya pili ni ile hatua
ya lava kwenye misuli na ubongo.
“Mtu anapokuwa na Lava hao kwenye
misuli wanakuwa kama mchelemchele yani vitu vyeupe vyeupe kwenye nyama na
vikiwa kwenye Ubongo wa ndio vinasababisha mtu kupata kifafa lakini wakiwa
minyoo tuu kwenye utumbo wanasababisha mtu kupata dalili zisizo za maalumu kwa
ugonjwa huo kama vile kupoteza hamu ya kula,tumbo kutokuwa vizuri kujisikia
kuharisha lakini haarishi yani ni kama dalili za mtu mwingine mwenye minyoo ya
kawaida” alifafanua Dkt. Ngowi.
Amesema takwimu nyingi ni zile za
mnyoo ambaye anakuwa nje ya utumbo kama vile kwenye Ubongo, Misuli, Moyo na
chini ya ngozi ambapo minyoo hukaa huko lakini kubwa zaidi takwimu zenyewe
zinatofautiana tofautiana kati ya Wilaya na Wilaya kulingana na namna jamii
inavyofuga nguruwe hao kwa kuacha watembee mitaani au kufugia ndani ambapo
kwenye takwimu kubwa ni Mbozi ambapo imefikia hadi asilimia 30%, Iringa 16.7%
ya maambukizi huku Kinondoni Jijini Dar es salaamu kwa wanaohudhuria kliniki ya
Kifafa asilimia 8% imesababishwa na uwepo wa Minyoo tegu kwenye Ubongo.
Aidha Dkt. Ngowi katika kumaliza
tatizo hilo amehimiza kufuatwa kwa mapendekezo yote ya utafiti huo ambayo
yamehimiza kukomesha ufugaji wa nguruwe na kuacha wajitafutie chakula mitaani
na kuwa na machinjio maalumu ya nguruwe ili nyama iweze kukaguliwa kabla ya
kwenda kuuzwa na kuchomwa.
Mradi wa CYSTINET Africa umefadhiliwa na Wizara
ya Elimu na Utafiti ya Serikali ya Ujerumani (BMBF) ambao umeratibiwa na SUA,
Mtandao huu unajumuisha Taasisi 5 katika Nchi Nne za washiriki ambazo ni SUA,
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu Tanzania, Chuo Kikuu cha Zambia Pamoja na Chuo Kikuu cha Eduardo
Mondlane - Msumbiji.
PICHA ZA WADAU WAKIFUATILIA MAWASILISHO KWENYE WARSHA HIYO.
0 Comments