SUAMEDIA

SUA yaishukuru Korea kwa ufadhili wa Mradi wa Vifaa vya Maabara

 

Adam Maruma - SUA

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), imeishukuru nchi ya Korea Kusini kupitia Shirika lake la KOICA, kwa ufadhili wa mradi wa vifaa venye uwezo wa kutunza wadudu  kwenye ubaridi ambapo vifaa hivyo vinatarajiwa kutatua changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo chuoni hapo  kwa wanafunzi  na watafiti.



Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika IPRB Korea Dkt. Hansol (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watafiti kutoka SUA (wa pili kutoka kushoto) ni Mkuu wa Idara ya Microbiolojia, Parasitolojia na Bioteknolojia Dkt. Augustino Chengula (Picha na Adam Maruma)

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo Mkuu wa Idara ya Microbiolojia, Parasitolojia na Bioteknolojia Dkt. Augustino Alfred Chengula amesema kwa awamu ya kwanza tayari chuo kimepokea hadubini 3 na wanataraji kupokea vifaa vingine katika siku zijazo.

‘’Tuna kila sababu ya kuwashukuru wenzetu hawa, kwa sababu wametuletea hadubini na pia watatuleta friza, na kamputa moja ambayo itakuwa msaada mkubwa sana kwa ajili ya kujifunzia wanafunzi wetu lakini pia kwa ajili ya kufanyia tafiti mbalimbali zinazohusisha wadudu wanaoathiri  wanyama na binadamu’’ anasema Dkt. Chengula.


Pichani ni hadubini 'Microscopy' zilizotolewa na KOICA ili zitumike kwenye mradi huo

Mkuu huyo wa Idara ameongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia wanafunzi wengi kujifunza kwa wakati mmoja kwa kuwa  sasa chuo  kinapokea idadi kubwa ya wanafunzi na pia walimu wanaofanya tafiti zao  vifaa hivyo vitawasaidia sana kufanya tafiti kwa urahisi zaidi.

Kwa upande wake kiongozi wa mradi huo wa kuhifadhi wadudu  ambae pia ni Mhadhiri chuoni hapo Dkt. Jahashi Nzalawahe amesema mradi huo unalenga kuboresha uhifadhi wa wadudu na utakua na awamu 4 na awamu ya kwanza itakua ni ukarabati  maabara ambazo zitatumika kufundishia wanafunzi haswa wanafunzi wa shahada ya Umahiri na Uzamivu  ambapo maabara 3 tayari zimekarabatiwa.

Dr. Nzalawahe amesema awamu ya pili ya mradi huo, ambayo inaendelea sasa ni kuanza kuziboresha maabara hizo kwa kuzipatia vifaa vitavyotumika katika kuwatambua wadudu hao pamoja na kuwahifadhi kwa muda mrefu kwa kuwa friza zitakazoletwa zitakuwa na uwezo mkubwa kwa kazi hiyo.

‘’Kilichofanyika leo ni wenzetu kutoka Korea ambao ndio wadau wetu katika mradi huu wamekuja kutukabidhi awamu ya kwanza ya vifaa ambavyo ni hadubini 3 ambapo hadubini 2 zitakuwa ma camera za kupiga picha  na kuzitunza kwenye computa na wanafunzi wataweza kuona kupitia computa hizo, na sio lazima kupitia kwenye hadubini zenyewe’’ amesema Dk. Nzalawahe

Mtafiti huyo kiongozi wa mradi amesema  awamu ya tatu ya mradi kuwa itajumuisha kuagiza vifaa ambavyo vitatumika katika ukusanyaji wa wadudu hao wa wanyama mbalimbali wafugwao na wanyama wa porini.

Amesema awamu ya nne ya mradi itakuwa ni kuagiza vifaa ambavyo vitatumika kufanyia ukusanyaji wa wadudu wa Wanyama mbalimbali wafugwao na waporini na awamu ya 4 ya mradi itakua ni wadudu hao kuhifadhiwa kwenye vifaa ambavyo vitaletwa kwa ajili ya kuhifadhia wadudu hao, anasema Dk. Nzalawahe

Nae Dkt. Hansol Park ambae Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika hilo  kutoka Korea amesema mradi huo ulianza mwaka 2021, na wameamua kuanzisha Benki hiyo ya wadudu SUA kwa ajili ya kusaidia kukusanya, kutafiti wadudu na kufugwa katika maabara hizo ili kusaidia wanafunzi na watafiti.

Post a Comment

0 Comments