SUAMEDIA

SUA yafanya mazungumzo ya makubaliano ya kushirikiana na Ufaransa

 

Na: Gladness Mphuru

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimeingia makubaliano ya ushirikiano na Ufaransa katika taaluma ili kubadilishana wanafunzi wa pande hizo mbili.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Esron Karimuribo (wa kwanza kushoto) pamoja na Prof. Jean-Luc Bosio (wa kwanza kulia) wakiwa katika mjadala wa makubaliano ya ushirikiano kati ya SUA na Ufaransa.

Hayo yamebainishwa Novemba 10, 2022 mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Esron Karimuribo, wakati akihitimisha ziara ya siku mbili ya wageni hao kutoka Taasisi za Elimu ya Juu nchini Ufaransa iitwayo L’Institut Agro Montpellier iliyofanyika katika Kampasi za Edward Moringe na Solomoni Mahlangu mkoani Morogoro.

“Hawa wenzetu wamekuja  ili kuanzisha maongezi jinsi ambavyo tunaweza kuwa na mashirikiano katika maeneo mbalimbali, kwa mazungumzo yetu maeneo makubwa ambayo tumekubaliana kushirikiana ni pamoja na kubadilishana wanafunzi wetu kutoka SUA Kwenda kwao na wao kuja kwetu” amesema Prof. Karimuribo

Prof. Karimuribo amesema kuwa wameshabihiana sana katika upande wa taaluma kwa sababu wamejikita zaidi kutoa mafunzo ya kilimo cha kitropikali ambacho kinafanana na chetu sambamba na kuboresha mahusiano ya wanasayansi, wanataaluma na wabunifu kutoka nchi zinazoongea Kifaransa na za Kingereza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mahusiano ya Kimataifa kutoka Taasisi hiyo Prof. Jean-Luc Bosio, amesema wamekuja kukitembelea Chuo cha SUA pamoja na vyuo vingine washirika kwenye Mradi wa Innoversity.


Kwa upande wake Meneja wa Mradi huo Bi. Trufina Matekele amesema mradi huo umefadhiliwa na ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kusaidia Vyuo Vikuu vitatu ambavyo ni SUA, Chuo Kikuu cha Iringa na Nelson Mandela African Institution of Sciences and Technology.

Mradi huo wa Ubunifu ‘Innoversity Project’ unalengo la kusaidia wanafunzi kuhakikisha mawazo yao ya kibunifu yanakuwa na tija wanapokuwa vyuoni na hata nje ya vyuo, kwa lengo la kupunguza ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu.



Post a Comment

0 Comments