Gerald Lwomile
Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa pamoja na kuwepo kwa muingiliano mkubwa wa dawa za binadamu na wanyama lakini si sahihi kwa dawa za binadamu kutumika kwa wanyama na dawa za wanyama kutumika kwa binadamu kwani ni moja ya chanzo cha usugu wa vimelea vya magonjwa.
Prof. Robinson Mdegela akisalimiana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulege (Picha Maktaba- Mtandao)
Hayo yamesemwa na Mhadhiri Mwandamzi kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Robinson Mdegela wakati akizungumza katika kipindi cha Malumbano ya Hoja kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha ITV.
Prof. Mdegela amesema viwango vya dawa
vilivyowekwa mfano kwenye dawa ya ‘Tetracycline’ kwa tiba ya mnyama ni
tofauti na viwango vilivyowekwa kwenye tiba ya binadamu na kuongeza kuwa dawa
hizi mbali na kutibu pia zina madhara hivyo kuzitumia kinyume na zilivyopangiwa
ni kuhatarisha maisha kwa kiumbe ambacho
hakikulengwa.
“Mazoea ni mabaya, tumeshuhudia sasa hivi
wafugaji wanadhani kuwa dawa ya binadamu iko kwenye kiwango kikubwa zaidi na wanadhani
dawa inayotumika kutibu magonjwa ya binadamu kule inafaa kumbe hapana” amesema
Prof. Mdegela.
Akizungumzia namna ya kuepuka matumzi holela ya
dawa ambayo yanaweza kusababisha usugu wa vimelea vya Magonjwa Mwenyekiti wa
Chama cha Wafamasia Tanzania Bw. Fadhili Hezekiah amesema zipo silaha mbili
kubwa zinazoweza kutumika katika kukabiliana na hali hiyo ambazo ni elimu na usimamizi
wa sharia.
Naye Bingwa wa Magonjwa ya Kuambukiza kutoka Chuo
Kikuu cha Buganda (CUHAS) Prof. Jeremiah Seni amesema kuna makundi ambayo yanaweza
kuathirika zaidi na usugu wa vimelea vya magonjwa kama Watoto ambao wako chini
ya miaka 5 ambapo mwaka 2009 walifanya utafiti na kugundua katika watoto 100
walio chini ya mwezi mmoja Watoto 19 walifariki.
Ameyataja makundi mengine kuwa ni pamoja na
wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, walioko katika chumba cha wagonjwa mahututi na
wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwili.
Usugu wa vimelea hutokea pale ambapo dawa
iliyokuwa ikiua aina fulani ya vimelea vya magonjwa ilipotumika awali kushindwa
kufanya kazi pale mgonjwa alipopata aina hiyo hiyo ya vimelea.
0 Comments