Na; Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Kitengo cha Mahitaji Maalum kilicho chini ya Mradi wa Kuendeleza Vyuo Vikuu ili kuleta Mabadiliko ya Kiuchumi nchini (HEET) kimeandaa zoezi la upimaji wa Usikivu Hafifu kwa lengo la kuwasaidia Wanajumuiya wa SUA hasa wanafunzi kuweza kutambua tatizo hilo na chanzo chake na namna ya kukabiliana nalo.
Hayo yamebainisha na Mratibu wa Kitengo hicho ambaye pia ni MhadhiriKitengo cha Mitaala na Ufundishaji Shule Kuu ya Elimu SUA Dkt. Tabitha Lameck Lupeja wakati akizungumza na SUA Media Kampasi ya Solomoni Mahlangu kwenye siku ya kwanza ya zoezi hilo.Dkt. Tabitha amesema katika kufanikisha zoezi hilo Chuo kimemualika Mtaalam wa Afya kutoka Wizarani ambaye atakuwepo kwa muda wa siku nne chuoni hapo kwa ajili ya kupima Kiwango cha Usikivu na kutoa ushauri kwa mtu mwenye tatizo la Usikivu Hafifu au anayehisi kuwa na tatizo hilo. |
Amesema mojawapo ya tatizo ambalo limekuwa likijitokeza hususani kwa wanafunzi wengi ni shida ya Usikivu ambayo inaathiri sana maendeleo ya mwanafunzi Kitaaluma na kumsababishia kutoweza kujifunza vizuri kama inavyotakiwa na kuhitaji uangalizi na umakini wa hali ya juu katika kujifunza kwake.
Dkt. Tabitha amesema mtu atakayepatikana na tatizo hilo la usikivu hafifu atapewa vifaa vinavyoitwa Hearing Aids ambavyo vitaweza kumuongezea Kiwango au Ufanisi wa kusikia ambapo kwa mtu asiyesikia atapewa mafunzo ambayo ni Leap Reading yatakayo msaidia kuangalia ishara katika mdomo na kuweza kujifunza.
Kwa upande wake Naibu Waziri Wizara ya Asasi, Jinsia na watu wenye Mahitaji maalum katika Serikali ya Wanafunzi SUASO Peter John amesema Serikali yao inatamani kuona kila mwanafunzi anafikia malengo yake katika masomo bila kujali changamoto aliyonayo.
Naye Simba Issah Mwanafunzi wa Shahada ya Awali ya Walimu wa Sayansi katika Masomo ya Kemia na Bayolojia ambaye ni miongoni mwa wahanga wa tatizo hilo amesema zoezi hilo lina msaada mkubwa kwao kwani baada ya kufanyiwa uchunguzi watapewa vifaa vya usikivu ambavyo vitawasaidia kusikia vizuri pindi wawapo darasani kwani awali ilikuwa ni ngumu kusikia kile anachofundishwa na b mwalimu anavyotamka maneno ndipo aelewe.
0 Comments