SUAMEDIA

MRADI WA CoForEST WAWEZESHA KUKAMILISHA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM

 Na: Calvin Gwabara

Mradi wa kuhifadhi misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya mazao ya misitu Tanzania (CoForEST) kupitia Uvunaji edelevu wa mazao ya misitu umewezesha Chama cha mapinduzi CCM kata ya Matuli Wilaya ya Morogoro kutekeleza Ilani na ahadi za uchaguzi kwa asilimia 90% kwa kuanzisha na kukamilisha miradi mitano ya maendeleo.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) kata kata ya Matuli Maalim Abdalah Semindu (kulia) akieleza mradi huo ulivyoleta maendeleo kwenye kata yake.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) kata kata ya Matuli Maalim Abdalah Semindu wakati ziara ya Wataalamu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wanaotekeleza mradi huo kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) walipotembelea vijiji vyenye miradi kuangalia mafanikio ya Mradi  tangu uanzishwe kwenye vijiji hivyo mwaka 2016.

Semindu amesema mwaka 2015 kwenye uchaguzi wakati akimnadi mgombea Udiwani wa kata hiyo Lucas Lemomo kupitia Ilani ya CCM kuomba kura aliahidi kutekeleza ilani ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa Zahanati,Barabara, Miradi ya Elimu na mingi ikiwemo maji safi na salama lakini hakujua vitapatikanaje lakini baada ya kuingia kwa Mradi huo Miradi yote inatekelezeka na kukamilika kabla ya muda alioahidi.

 “Mimi mkaa endelevu naueshimia kwelikweli, sababu umenivika nguo, nilipoahidi 2015 kuwa nitawaletea maendeleo, maendeleo yamebebwa na mkaa endelevu, nilisema, mchagueni Diwani wangu na chama change cha CCM tutafanya mambo moja, mbili, tatu, nikiwa sijui nafanyaje, lakini baada ya mkaa endelevu ahadi zote nimezitimiza, nadaiwa madeni madogo madogo , na ikifika 2023 nitamaliza madeni yote katika kata yangu” alisema Semindu.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Matuli Lucas Lemomo ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kupitia Vijiji vitatu vya Diguzi,Matuli na Lulongwe vinashitekeleza mradi huo vimeweza kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi milioni 250 kitu ambacho haikuwezekana Kijiji kuweza kuwa na mapato yanayofikia milioni 100 kwa mwaka lakini kupitia Usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji na uvunaji endelevu wa mazao ya misitu hususani Mkaa imewezekana.

Diwani wa kata ya Matuli Lucas Lemomo ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro akieleza namna mradi huo ulivyonufaisha kata yake.

Amesema Kijiji cha Diguzi kilipata shilingi milioni zaodi ya 80, Matuli shilingi zaidi ya milioni 104 na Lilongwe zaidi ya shilingi milioni 100 ambazo zimetekelza miradi mbalimbali kwenye vijiji hivyo ikiwemo Ujenzi wa Zahanati, Ujenzi wa madarasa, Matundu ya Vyoo, Nyumba ya Walimu ya mbili kwa moja, Kulipia Bima ya afya wanakijiji pamoja na ukarabati wa kisima cha maji cha bomba la kupampu (Mdundiko).

Mhe.Limomo amesema jambo kubwa ambalo wanajivunia sana wananchi na viongozi wa vijiji na kata ni Mradi kuwezesha kuanzishwa kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao umewasaidia pia kuanzishwa kwa masijala nzuri ya ardhi na kupatiwa hati za kimila za mashamba na viwanja vya makazi na hivyo kumfanya kila mwananchi kuwa na uhakika nae neo lake.

“Kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi sasa Kijiji kitumia asilimia 10% ya misitu huku asilimia 90% ikibaki chini ya Kijiji na kulindwa, hili ni fanikio kubwa maana tumedhibiti uchomaji hivyo wa mikaa na ingakuwa zamani hiyo barabara yote mliyopita mngekutana na pikipiki zilizobeba magunia ya mkaa zikiwa zimeongozana lakini kwa sasa biashara hiyo haipo inafanywa kwa utaratibu mzuri wa uhifadhi kwa uendelevu” alifafanua Limomo.

Mradi wa CoForEST unatekelezwa katika vijiji kadhaa vilivyopo kwenye wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro, Liwale, Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi na Kilolo mkoani Iringa.

Zahanati ya Kijiji cha Lulongwe iliyojengwa kutokana na mapato ya mkaa endelevu.

Nyumba ya Walimu ya Mbili kwa moja iliyojengwa kwa kupitia Mapato yatokanayo na mkaa endelevu.

Wajumbe wa kamati ya maliasili ya kijiji pamoja na wajumbe wa Kijiji wakifuatilia Mkutano huo.

Washiriki wa mkuatano huo wakifuatilia shuhuda



Post a Comment

0 Comments