SUAMEDIA

MISITU IKITUNZWA NA KUVUNWA KWA UENDELEVU NI KIWANDA - SIANGA


Na: Calvin Gwabara 

Serikali,Wadau wa Misitu na Jamii kwa ujumla wametakiwa kutambua kuwa Misitu ni Kiwanda kwa kuwa inaweza kuchangia katika kutoa ajira na fursa zingine pale itakapotunzwa na kuvunwa kwa uendelevu ili kutoa ajira kwa kizazi hiki na kijacho.

 Bwana Cassian Sianga ambaye ni mratibu wa Kikosi kazi cha Misitu Tanzania (TFWG) wakati akizungumza na Waandishi wa habari (Hawapo pichani) nje ya Mkutano huo.

Kauli hiyo imetolewa na Bw. Cassian Sianga ambaye ni Mratibu wa Kikosi kazi cha Misitu Tanzania (TFWG) wakati akizungumza na Wadau wa Misitu kutoka Serikalini, Mashirika yasiyo ya Kiserikali zaidi ya kumi pamoja na Waandishi wa habari kwenye mkutano uliolenga kuangalia masuala ya utawala bora wa usimamizi wa misitu Tanzania.

“Misitu tusiichukulie kama misitu tuu bali tuichukulie kama kiwanda  ukiangalia kutoka kwenye shamba wanapovuna mpaka kwenye soko inatoa ajira nyingi sana lakini tukiendelea na kutoa matamko,sharia na kanuni ambazo zitaleta matatizo kwenye mnyororo mzima wa thamani wa biashara ya mazao ya misitu tutaanza kuzalisha vijana ambao hawana kazi ukiangalia wanaopakia kwenye magari,wanaofungasha na wakinamama wanaouza wote watakosa ajira”alieleza Bwana Sianga.

Kwa upande wake Afisa majadiliano na Sera wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Mistu Tanzania (MJUMITA) Bi. Elida Fundi amesema MJUMITA kwa kushirikiana na TFCG wamekuwa wakisaidia Wananchi waishio maeneo yenye Misitu kutengeneza mpango wa matumizi bora ya ardhi na usimamizi shirikishi wa misitu ili kuweza kulinda misitu hiyo iliyo ndani ya ardhi za vijiji na kuvuna Mkaa na mbao kwa njia endelevu.

 Afisa majadiliano na Sera wa Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) Bi. Elida Fundi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) nje ya mkutano huo.

Mbinu hii sisi tunaiona kuwa ni nzuri kwamaana Misitu ile imekuwa chini ya Wananchi wakiilinda wao wenyewe na kuivuna na kunufaika kutokana na ulinzi wanaoufanya maana wanaona ina manufaa kwao kuliko tukiiacha kama shamba la bibi na tunaamini mikaa hii mingi inayovunwa kuelekea mijini inavunwa kwenye maeneo holela yanayovunwa hovyohovyo na ambayo hayajahifadhiwa kisheria” alieleza Bi Elida Fundi.

Aliongeza “Tunatamani Serikali iwekeze na kuhamasisha kwa kuwasaidia Wananchi waweze kuhifadhi Misitu yote iliyo kwenye ardhi za vijiji iwekwe chini ya mamlaka za vijiji waweze kuihifadhi na kuitumia kwa njia endelevu kama ambavyo tumeona Vijiji vimejenga Shule, Zahanati, huduma za maji,kulipia Bima ya afya wanakijiji wake na nyingine nyingi ambazo zilikuwa zifanywe na Serikali lakini kubwa Misitu yao wanailinda wenyewe”.

 Amesema MJUMITA inatamani Wananchi waweze kuilinda na kuhifadhi Misitu yote iliyo kwenye ardhi za vijiji ili waweze kunufaika na faida zitokanazo na mazao ya misitu.

Elida amesema hali ni tofauti kwenye vijiji ambavyo havina mpango huu wa usimamizi shirikishi wa Misitu ya vijiji maana Misitu hailindwi na Wananchi na hivyo wanachoma mikaa na kukata mbao kwa njia zisizo endelevu na mazao hayo husafirishwa kwa njia za panya na kuikosesha Serikali mapato.


PICHA ZA WADAU MISITU WAKIFUATILIA MKUTANO HUO WA KIKOSI KAZI CHA MISITU TANZANIA (TFWG)











Post a Comment

0 Comments