Na
Gerald Lwomile
Kibaoni
- Mpimbwe
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wametakiwa kutumia muda wao vizuri, kujiheshimu kuwa na nidhamu na kuhakikisha
wanajitolea katika masomo wakati wote jambo litakalowasaidia kufikia malengo au
ndoto zao.
Wanafunzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda wakiwa katika Picha ya pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda (aliyevaa miwani katikati) wa pili kutoka kushoto (waliokaa) ni Dkt. Nyambilila Amuri Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Awali SUA
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada
za Awali kutoka SUA Dkt. Nyambilila Amuri wakati akizungumza na wanafunzi wa
Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo wilaya Mpimbwe Mkoani Katavi wakati wa ziara
ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda.
Dkt. Nyambilila amesema wakati mwingine vijana wengi
wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kushindwa kukubali kufuata
miongozo na kanuni za mahali husika na kujikuta wakifanya mambo ambayo
huwapotezea muda ikiwa na pamoja na kujiingiza katika makundi hatarishi.
Amesema masomo ambayo mwanafunzi amekuja kusoma katika
Chuo hicho ni mwanzo muhimu wa kutengeneza kesho yake ikiwa ni pamoja na
kujijengea uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali zinamzunguka akitumia elimu
aliyoipata.
Mkurugenzi huyo katika Kurugenzi ya Shahada za Awali
amesema, endapo mwanafunzi atayachukulia kwa umuhimu unaostahili masomo yake
basi taifa litajenga wataalamu wazuri ikiwa ni pamoja na wanasayansi vijana mahili.
Katika hatua nyingine Dkt. Nyambilila amesema
Kurugenzi ya Shahada za Awali, Wanataaluma na Menejimenti ya Chuo hicho
itahakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha na kuwawezesha wanafunzi kuhakikisha
wanapata kile kilichowaleta chuoni hapo ambacho ni elimu na maarifa katika fani
walizozichagua.
Amesema, katika kuhakikisha wanafunzi wanafikia
malengo yao watahakikisha wanaendelea kuboresha mazingira ya mwanafunzi
kujifunzia katika Kampasi zote na kuhakikisha wanatoa ushauri kwa wanafunzi
kuhusiana na shahada mbalimbali walizochagua.
0 Comments