SUAMEDIA

SUA yatenga Bilioni 20 kupanua na kuboresha Kampasi ya Mizengo Pinda

 

Na Gerald Lwomile

Katavi

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa ‘HEET’imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 20 ili kufanya upanuzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo wilayani Mpimbwe mkoani Katavi.


Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda (kushoto) akikaribishwa na Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani 

Akizungumza wa wanafunzi wanaosoma katika Kampasi hiyo Novemba 08, 2022 Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema fedha hizo zitaboresha mazingira ya wanafunzi kujisomea chuoni hapo na kuleta fursa mbalimbali katika wilaya ya Mpimbwe na mkoa wa Katavi.

Prof. Chibunda amesema kupatikana kwa fedha hizo kutapunguza baadhi ya changamoto kwani chuo kinatarajia kujenga bweni la wananfunzi ambalo litachukua wanafunzi kati ya 700 hadi 1000 na kujenga eneo la wanafunzi kujipatia chakula ambapo zaidi ya wanafunzi 400 wanaweza kukaa na kula kwa wakati mmoja.


Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda

Aidha Makamu Mkuu huyo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amesema kupitia bajeti ya chuo wamepanga kununua basi moja kubwa la kutosha kubeba watu 65 ili hata ikitokea wanafunzi wanataka kwenda katika mazoezi kwa vitendo waende kwa urahisi zaidi.

Katika hatua nyingine Prof. Chibunda amewata wanafunzi kuweka bidii kubwa katika masomo yao na kujiepusha na makundi ambayo yanaweza kusabababisha kutofikia ndoto zao.

Awali akimkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo, Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani amesema miradi mbalimbali ya uboreshaji wa mazingira katika eneo hilo inaendelea ambapo hivi sasa wanachimba kisima kikubwa cha maji ili kutosheleza mahitaji ya maji kwa wanafunzi na watumishi.

Aidha amesema  sasa wana jenereta kubwa la kufua umeme ambalo limepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la umeme ambalo limekuwa likiwakabili kutokana na kukatika umeme mara kwa mara.


Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Awali Dkt. Nyambilila Amuri aliyevaa miwani akiwa na watumishi wengine ambao ni sehemu ya ujumbe wa Makamu Mkuu wa Chuo wakiwa ziarani katika Kampasi hiyo

Baadhi ya wanafunzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda wakimsikiliza Makamu Mkuu wa Chuo (hayupo pichani)


Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani  (kulia) akitoa maelezo ya namna watajenga baadhi ya majengo kwa Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda



 Uchimbaji wa kisima kikubwa cha maji kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na watumishi ukiendelea katika Kampasi ya Mizengo Pinda 


Post a Comment

0 Comments