Na Amina Hezron, Morogoro
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaomba wataalamu
kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kuzidi kufanya tafiti juu ya mbegu
za miti rafiki wa maji ili zikazalishe miche itakayosaidia katika utunzaji wa vyanzo
vya maji vilivyoathirika.
Dkt. Jafo ameyazungumza hayo Novemba 24, 2022 mjini Morogoro
wakati wa Majalisi ya SUA yaliyofanyika katika Kampusi Kuu ya Edward Moringe
ambapo amesema wataalamu waangalie miti ya asili yenye sifa ya kuhifadhi maji
ikatumike katika kurejesha uhalisia wa mito katika baadhi ya maeneo.
“Mbinu ambayo nimefikiria ni kuzifanya shule zetu za msingi na sekondari ziwe vituo vya kuzalishia miche ili iwe rahisi kwa maeneo mengi kupata miche hiyo lakini changamoto ni upatikanaji wa mbegu hivyo tafiti ziendelee kufanyika ili mradi tuweze kupata mbegu za kutosha na kwa gharama nafuu zitakazosaidia kuikoa nchi”, alisema Dkt. Jafo.
Aidha Dkt. Jafo ameipongeza SUA kwa tafiti zake ambazo zinafanya kilimo kuwa
na tija na kutoa mchango mkubwa katika Sekta ya Kilimo nchini na amewataka
wahitimu wanaohitimu masomo yao wanapopewa nafasi ya kazi basi kwenda kufanya
kazi kwa juhudi na maarifa ili kuzijengea heshima Taasisi zilizowajengea maarifa.
“Kwa kuwa mnalipwa mshahara basi nendeni mkafanye kazi na
kuacha uvivu kafanye kazi asipatikane wa kuvaa viatu vyako utakapoondoka, mfanye
kazi kama ibada kwamba usipotimiza wajibu wako mungu atakuhukumu kwa kuwa kuna watu
wanahitaji msaada mkubwa sana hivyo wewe msomi umepata fursa basi wasaidie”,
alisema Dkt. Jafo
0 Comments