Na: Calvin Gwabara - Dodoma.
Matokeo yaliyojitokeza kwenye vijiji 41 vilivyokuwa vinatekeelza Mradi wa kuhifadhi misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya mazao ya misitu Tanzania (CoForEST) yamethibitisha kuwa Vijiji vinao uwezo wa kulinda,kusimamia misitu yao endapo vitanufaika na rasilimali hiyo.
Mwakilishi wa Balozi wa Uswiss Bi. Clara Melchior akitoa salamu za Balozi wa Uswiss kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau. |
Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Balozi wa Uswiss Bi. Clara Melchior kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau waliokuwa wanatekeleza mradi huo kuangalia matokeo yake na kujadiliana namna ya kutafuta fedha kwaajili ya kutekeleza mradi huo kwenye mikoa mingine ambayo haijafikiwa.
“Tumefanya awamu ya kwanza na awamu ya pili ya mradi na tumeona lengo
la mapato kwenye vijiji na mtu mmojammoja kumewezesha jamii kuona misitu hiyo
ni mali yao na hivyo kuhakikisha wanailinda,kuisimamia na kuivuna kwa njia
endelevu na hii inakwenda sambamba na swala la ugatuzi wa madaraka kwa Serikali
za vijiji kupewa mamlaka ya kupanga na kuamua mambo yao” alifafanua Clara.
Aidha ameongeza kuwa wameona bunifu mbalimbali ambazo zimepelekwa na mradi kwenye vijiji katika kusimamia misitu na kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya misitu yamepokelewa kwa mtazamo chanya zaidi na yameonesha kuwa na faida tofauti na awali ambapo wamekuwa wakifanya kienyeji au kwa mazoea.
Muwakilishi huyo wa balozi wa Uswiss ameiomba Serikali sasa kuongoza jitihada hizo nzuri zilizofanywa na mradi huo huku wao kama wadau wakae nyuma ya Serikali katika utekelezaji wa mpango huo hasa kwa kupeleka mbinu hiyo kwenye vijiji kwenye Mikoa mingine Tanzania.
Akitoa salamu za Wizara ya Maliasili na Utalii wakati akifungua rasmi mkutano huo Mkurugenzi wa idara ya Misitu na Nyuki Bwana Deusdedit Bwoyo amepongeza kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na mradi huo wa CoForEST na kuahidi matokeo na mbinu hiyo Serikali itaendelea kuieneza na kuitumia katika kulinda misitu nchini.
Mkurugenzi wa idara ya Misitu na Nyuki Bwana Deusdedit Bwoyo akifungua Mkutano huo wa wadau wa Mradi wa CoForEST jijini Dodoma. |
Amesema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania imebarikiwa na kuwa na misitu takribani milioni 48.1 kiasi ambacho ni sawa na asilimia 5 ya ardhi yote ya Tanzania huku kila mwaka nchi ikipoteza takribani hekta 469,000 kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kilimo.
“Misitu hii ikisimamiwa vizuri ni chanzo muhimu sana cha kuleta mapato vijijini lakini pia sekta ya misitu iliyosimamiwa Madhubuti na kwa uendelevu italeta mchango chanya kwenye sekta zinazotegemea ikolojia ya misitu ya asili kama vile kilimo, Maji, Wanyamapori na nishati”alifafanua bwana Deusdedit.
Amesema katika utafiti uliofanywa na wizara hiyo kwenye kuangalia mchango wa jumla wa misitu kwenye uchumi wa taifa umebainisha kuwa Misitu inachangia takribani trilioni 4.65 kwa mwaka na hivyo kuchangia asilimia 3.3 ya pato la taifa.
“Sisi watu wa taaluma ya Misitu tunatambua kuwa msitu unapaswa kuvunwa unapokuwa tayari lakini sasa kumekuwa na uvunaji holela wa misitu yetu kimsingi tusipochukua hatua sasa misitu hii itapotea na vizazi vyetu havitarithi kitu maana kauli mbiu ya Wizara ni tumerithi na tuwarithishe”alieleza bwana Deusdedit.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa TFCG bwana Charles Meshack amesem tafiti zinaonesha kuwa kilimo cha mazao kinachangia kwa asilimia 89 ya upotevu wa maeneo ya misitu yanayotoweka kati ya waka 2010 na 2017 na hivyo kukifanya kilimo kuwa chanzo kikuu cha kutoweka kwa misitu Tanzania.
Mkurugenzi mtendaji wa TFCG bwana Charles Meshack akichokoza majadiliano kwenye mkutano huo (kulia kwake ) ni Afisa maliasili wa Mkoa wa Morogoro bwana Joseph Chuwa. |
“Kama ardhi ya misitu itaendelea kubadilishwa kuwa mashamba ya kilimo hapatakuwa na misitu kwenye ardhi za vijiji ifikapo mwaka 2050 – 2070 na hii itakuwa na matokeo hasi kwenye vyanzo vya maji,udongo,bionuawai,mabadiliko ya tabia nchi na uchumi”Alifafanua Bwana Meshack.
Mradi wa CoForEST unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) katika vijiji 41 vilivyopo kwenye wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro, Liwale, Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi na Kilolo mkoani Iringa.
PICHA ZINGINE NI WADAU WA MKUTANO HUO WAKIFUATILIA MADA ZILIZOKUWA ZINAWASILISHWA.
0 Comments