Na: Calvin Gwabara - Mvomero.
Wakazi wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambao ni jamii ya
kabila la Wanguu waaachana mila za ubaguzi na ukatili wa kijinsia katika
ushiriki wa Wanawake kwenye majadiliani na kupanga mipango ya maendeleo baada
ya elimu ya Jinsi na Jinsia iliyotolewa na Mradi wa kuhifadhi misitu kwa
kuwezesha biashara endelevu ya mazao ya misitu Tanzania (CoForEST).
Bwana Ally Semwali ambaye ni mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Msolokelo kata ya Pemba na mtoa elimu ya masuala ya Jinsi na Jinsia. |
Ushuhuda huo umetolewa na Ally Semwali ambaye ni mjumbe wa Serikali
ya Kijiji cha Msolokelo kata ya Pemba na mtoa elimu ya masuala ya Jinsi na Jinsia
na kuthibitishwa na Wanawake wenyewe wakati wakizungumza na waandishi wa habari
kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini walipotembea Kijijini hapo viongozi
wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na
Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wanaotekeleza mradi
huo kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) kuangalia
mafanikio ya tangu ianzishwe.
Bwana Semwali amesema mfumo dume kwenye Kijiji hicho
umetoweka kwa asilimi zaidi ya 75% baada ya mafunzo ya mara kwa mara ya
kujengea uwezo jamii na kuwawezesha Wanawake kujiambua na kupaza sauti zao na
kukataa ukandamizi kwenye kaya na jamii nzima ya kabila la Wanguu.
“Kipindi cha nyuma sisi wanguu ni vigumu sana kwa mwanamke
kusimama mbele ya halaiki ya wanaume iwe kwenye mikutano ya Kijiji au familia kutoa
kauli, kusikilizwa na kupewa umuhimu kwa mawazao yake, lakini baada ya elimu
hali imebadilika kwa kiasi kikubwa sana maana sasa wanaongea kwenye mikutano kama
hivi,wanasikilizwa, wanashiriki katika shughuli za uchomaji mkaa tena huko ndio
wengi kuliko wanaume na kujipatia fedha na kupanga matumizi ya fedha
wanazozipata na waume zao’’ alifafanua Bwana Semwali.
Aidha amebainisha kuwa hali hiyo pia imebadilika kwa wanaume
pia maana huko nyuma kuna kazi ambazo mwaume alikuwa hawezi kuzifanya kwenye
nyumba kama vile kupika,kufua na nyinginezo lakini sasa wanashiriki vizuri na
hivyo kusaidiana katika kutekeelza majukumu mbalimbali ya familia na yale ya
kimaendeleo.
Kwa upande wake Stamili Kisingeli mkazi wa Kijiji cha
Msolokelo ambaye ni mnufaika wa Mradi na mafunzo hayo amesema kuwa wakati
maafisa wa MJUMITA NA TFCG wanaanza mafunzo hayo hali ilikuwa mbaya sana
wanawake waliojiona hawana thamani sana kwa jamii mbel ya wanaume lakini baada
ya mradi kuanza kuwashirikisha kwenye mikutano na kuwataka kuongea jamii
ikabadilika thamani yao ikaanza kuonekana.
Bi.Stamili Kisingeli mkazi wa Kijiji cha Msolokelo ambaye ni mnufaika wa Mradi na mafunzo hayo ya Jinsi na Jinsia. |
“Kwahiyo tupokuwa tunashiriki mikutano na wakufunzi kuhimiza
uwiano kwenye mafunzo na mikutano woga ukaanza kuisha maana kila wakija
wanauliza mbona jinsi ndogo na hata nyinyi mlipofika hapa mkauliza swali
hilohilo mbona jinsi ndogo? Kwahiyo tumejikuta tunazoea na wanaume wanazoea na
ukiingia kwenye shughuli za mkaa wanawake ndio wengi kuliko wanaume” alifafanua
Bi Kisingeli.
Aliongeza “Tuashukuru sana kwa kuja kwa huu mradi umetusaidia
sana maana sasa wanawake tunajiona kabisa kuwa tunaweza kumili na tunauwezo wa
kufanya kitu, kwa mfano mimi nimechoma mkaa na kufuga nyuki nimepata hela
nimesomesha Watoto wangu wawili shule ya Sekondari na nimenunua ng’ombe yani
tunajisikia raha kwakweli” alisema Kisingeli.
Bi. Kisingeli amesema pia kupitia biashara ya uchomaji wa
Mkaa endelevu Wanawake wengi sasa wamejiunga kwenye vikundi vya kuweka na
kukopa na kujipatia fedha za kuendesha Maisha yao na familia zao nah ii ni
matokeo ya elimu ya jinsi na jinsia kwenye Kijiji hicho.
Mradi wa kuhifadhi misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya
mazao ya misitu Tanzania (CoForEST) unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu
ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa
Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na ushirikiano
la Uswisi (SDC).
Afisa habari na Mawasiliano wa TFCG Bi. Bettie Luwuge akifafanua jambo mbele ya mkutano huo. |
Afisa Sera na Majadiliano wa Mtandao wa MJUMITA Bi. Elida Fundi akieleza lengo la ziara hiyo kwenye mkutano huo. |
0 Comments