SUAMEDIA

NGUVU IONGEZWE KWENYE KULINDA MISITU YA VIJIJI KWA KUHAMASISHA USIMAMIZI NA UVUNAJI ENDELEVU

 Na: Calvin Gwabara - Morogoro.

Imeelezwa kuwa asilimia takribani 50 ya misitu ambayo ipo kwenye ardhi za vijiji nchi nzima ipo hatarini kutoweka kutokana na uvunaji na uharibifu mkubwa wa misitu hiyo na hivyo kupelekea hatari ya Tanzania kuwa Jangwa.

Afisa maliasili wa Mkoa wa Morogoro Bwana Joseph Chuwa wakati akiongea na Waandishi wa Habri ofisini kwake.

Tahadhari hiyo imetolewa na Afisa maliasili wa Mkoa wa Morogoro Bwana Joseph Chuwa wakati akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake walioambatana na Wataalamu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wanaotekeleza mradi huo kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) wakati wakifuatilia kuangalia mafaniko ya Mradi huo toka kuanzishwa kwake na mipango ya Serikali na Jamii katika kuendeleza mafaniko hayo.

“Ukiangalia Misitu iliyo chini ya vijiji ni takribani asilimia 50 na inatoweka kila siku kutokana na uvunaji usiozingatia uhifadhi na uendeevu wake tofauti na ile iliyo chini ya Serikali kuu ambayo inalindwa na kusimamiwa vizuri kisheria na Serikali hivyo ni vyema misitu hiyo itambulike vizuri na iwekwe kwenye mpango bila hivyo kwa kasi hii tunayoiona kila siku ya uharibifu nchi yetu inaweza kuwa jangwa” alifafanua Chuwa.

Aidha ameeleza kuwa Mkoa wa Morogoro una jumla ya misitu 129 yenye jumla ya hekta 262,524 na mapato yaliyotokana na misitu kwa mwaka 2021/2022 ambayo yaliingia Serikali kuu ni shilingi bilioni 2.4 ambazo zimetoka kwenye vijiji 35 tu na vyenyewe vimepata kiasi cha shilingi Bilioni 1.6 tu ambazo zimetumika kutekeleza miradi yao mbalimbali ya maendeeo.

Afisa maliasili huyo wa Mkoa wa Morogoro amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Shirika la TFCG na Mtandao wa MJUMITA katika kuwezesha kuto elimu ya usimamizi shirikishi wa Misitu na Uvunaji endelevu wa misitu katika vijiji 35 pamoja na uanzishwaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Halmashauri ya Mvomero,Morogoro na Mvomero na kupitia Mradi wa Usimamizi shirikishi wa misitu ya Jamii (USMJ) chini ya Mradi wa kuleta mageuzi katika ya mkaa Tanzania (TTCS) .

Amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika Mradi huo hasa baada ya jamii kuweza kutambua namna inavyoweza kunufaika na misitu inayowazunguka kwa kuivuna kwa uendelevu na hivyo kupata motisha ambayo imesaidia kuimarisha misitu na nchi zingine kama vile Zambia kuvutiwa kuja Tanzania kujifunza mbinu hiyo.

Chuwa amesema hivi sasa Tanzania imeanza mkakati wa kupunguza tungamotaka (Mkaa na Kuni) kwa kuongeza matumizi ya Nishati safi kwa maana ya Umeme na Gesi lakini mpango huo hauwezi kusitisha matumizi ya mkaa kwa ghafla hivyo kwakuwa bado itaedelea kutumika kwa kupungua kidogokidogo lazima mkaa huo upatikane bila kuharibu misitu.

Wakizungumzia lengo la ziara hiyo ya kutembelea maeneo ya mradi wakiwa kwenye Kijiji cha Lulongwe  Afisa habari wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) Bettie Luwuge na Afisa Sera na Mjadiliano wa  Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) Elida Fundi wamesema ni kutaka kueneza elimu kwa wananchi wengine walio kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa na mradi ili viweze kuona na kujifunza na kuanzisha mbinu hiyo kwenye vijiji vyao.

Afisa habari wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) Bettie Luwuge akieleza malengo ya ziara hiyo kijijini hapo.

“Kuna mambo mazuri sana chanya ambayo Jamii na Viongozi wa wameyasimamia na kuyatekeleza hapa kwenye kijiji cha Lulongwe tangia mradi huu uanze ambayo jamii na viongozi kwenye vijiji vingine nchini wanaweza kujifunza na kuweza kusaidia kutunza misitu yao na wao kunufaika kama ambavyo mmenufaika na hivyo kuitunza misitu yetu nchini kote kwa faida yet una vizazi vijavyo” Alieleza Bettie.

Amesema TFCG na MJUMITA ni moja ya wadau ambao wanashirikiana na Serikali katika kuteleza sera ya misitu nchini hivyo wanapambana kwa njia mbalimbali katika kuhakikisha kuwa elimu inafika kwenye maeneo yote nchini lakini mchango wao kama wadau unaonekana na kuendelezwa.

Aidha amesema mradi unamaliza muda wake wa utekelezaji lakini wanatamani kuona kuwa mafunzo waliyotoa na uwezo uliojengwa kwa wananchi na viongozi unaendelea kuishi katika miyo yao na hivyo mfumo huo wa usimamizi shirikishi wa misitu na uvunaji endelevu wa rasililimali za misitu unaendela na kuleta faida kwa Taifa na jamii nzima.

Kwa upande wake Afisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA bi Elida Fundi amesema katika kipindi chote cha mradi kuna mambo mengi yamefundishwa ambayo yameleta faida kwao lakini pia wamepitaia changamoto mbalimbali katika utekelezaji wao hivyo ni vyema wakapaza sauti zao ili kusaidia wengine.

Afisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA bi Elida Fundi akifafanua jambo kwenye mkutano huo.

“Kupitia utekelezaji baada ya mafunzo kuna changamoto mbalimbali mmekumbana nazo ni kwa namna gani mmeweza kuzitatua hadi kufikia mafanikio haya leo ili tuweze kujifunza na kuwaambia wenzetu kwamba hili linawezekana na linaweza kufanyika vizuri kwa namna hii” alibainisha Elida.

Mradi wa CoForEST unatekelezwa katika vijiji kadhaa vilivyopo kwenye wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro, Liwale, Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi na Kilolo mkoani Iringa.

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Bwana Joseph Chuwa.

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Bwana Joseph Chuwa.



Post a Comment

0 Comments