SUAMEDIA

Wahitimu 3,744 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo watunukiwa vyeti vya kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu

 

Na Hadija Zahoro, Morogoro

Jumla ya Wahitimu  3,744  wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA ) kutoka program 59 wametunukiwa vyeti vya kuhitimu  elimu ya Chuo Kikuu wakiwemo Wanaume  2,223 na Wanawake 1,479.


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba (wa pili waliokaa ) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman (wa tatu kulia waliokaa) na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda (wa kwanza kulia waliokaa) na viongozi mbalimbali na wanataaluma wa chuo hicho


Akitaja takwimu za Wahitimu katika Mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Michezo vya Kampasi Kuu ya Edward Moringe ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema idadi ya waanawake waliohitimu ni  sawa na asilimia 39.9.  

Katika takwimu hizo wahitimu  3,425 ni kutoka Shahada za Kwanza ambapo wanaume ni 2,083 na wanawake wakiwa 1,342, Shahada za Umahiri wahitimu 41  wanaume  23 na wanawake 18, Stashahada ya Juu ya Elimu wahitimu wawili mwanamke 1 na mwanaume 1, Shahada za Uzamivu 9, wanaume 8 na mwanamke 1 ,wahitimu wa Stashahada 220 wanaume 121  na wanawake 99 pamoja  na wahitimu 48  wa Astashahada wakiwemo  wanaume  29  na  wanawake 19. 

Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda akitoa taarifa ya chuo kwenye mahafali hiyo

Ameeleza kuwa  idadi ya wahitimu kwa mwaka wa masomo 2021/2222 imeshuka kutoka  wahitimu 4,078  wa mahafali ya mwaka uliopita  2020/21 hadi kufikia idadi  ya  3,744, kwakuwa wengine walihitimu katika Mahafali ya Katikati ya  Mwaka yaliyofanyika  mwishoni mwa mwezi Mei  mwaka huu.

Aidha, Prof. Chibunda ameeleza kuwa Mafanikio ya mwaka hadi mwaka ya Chuoni hapo yanatokana na juhudi za Wanataaluma kwa kushirikiana na wazazi na walezi pamoja na wanafunzi wenyewe ambapo pia amewataka wahitimu kuonesha juhudi  na uaminifu huko watakapoenda baada ya kuhitimu masomo yao kama walivyoonesha wakati wakiwa Chuoni.

‘‘Mahafali ni tukio la kipekee sana popote pale Duniani kwa wahitimu, tukio hili ni muda mahsusi wa kusheherekea,  ni muda pekee wa kutathmini na kutafakari mafanikio ya miaka kadhaa katika kufikia  malengo waliojiwekea, juhudi walizozionesha katika masomo yao ,uaminifu  na moyo wa kusoma na kufanya kazi waweze kuonesha katika mahala pao pa kazi”, ameeleza Prof. Chibunda

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo( SUA)  Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, ameeleza kuwa Sherehe hiyo ya Mahafali ni uthibitisho dhahiri wa mchango mkubwa katika utekelezaji mzuri wa majukumu ya Chuo.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo( SUA)  Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman akizungumza katika mahafali hiyo

Amesema ili kutoa mchango wa kuiwezesha Tanzania kutekeleza Malengo endelevu ya maendeleo  mwaka 2016 na 2030, Chuo kinaendelea  kutilia mkazo katika kutoa elimu bora kwa wahitimu wake  kwa kuhakikisha kwamba kuna Sera na miongozo  stahiki ya kusimamia ubora wa elimu Chuoni.







Picha zikiwaonesha wanataaluma na wanafunzi mbalimbali waliokuwa kwenye mahafali hiyo

Post a Comment

0 Comments