SUAMEDIA

SUA anzisheni Kanzidata ya wanafunzi waliofaulu vizuri - Dkt. Francis Michael

 

Na Amina Hezron, Morogoro

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt Francis Michael ameshauri vyuo vikuu nchini kuwa na Kanzidata maalumu kwa ajili ya wanafunzi waliofanya vizuri  kwenye masomo yao ili zinapotoka nafasi za ajira kwenye taasisi mbalimbali waweze kupewa kipaumbele katika ajira.




Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt Francis Michael akizungumza na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao (hawapo pichani)

Dkt Francis Michael ameyasema hayo leo  Novemba 24, 2022 mjini Morogoro wakati wa Majalisi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) yaliyofanyika katika Kampusi Kuu ya Edward Moringe ambapo amesema zoezi hilo litasaidia nchi kuwa wataalamu bora.

“Utaratibu huo ulikuwepo toka zamani lakini zoezi hilo lilisimama kutokana na utaratibu mpya wa ajira ulioletwa lakini nafikiri ni wakati muafaka sasa tuangalie utaratibu mzuri wa kuwafanyia hivyo ili tusiwapoteze mtaani ukizingatia wengine wapo katika taaluma ambazo ni haba ambazo tunaishia pengine kuwatafuta kutoka nchi za nje”, amesema Dkt Francis Michael.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amewataka wanafunzi wenye jinsia ya kiume kuimalisha nidhamu katika masomo yao ili kupata matokeo mazuri ambayo inaonekana kwa nafasi kubwa kubebwa zaidi na wanafunzi wenye jinsia ya kike.







Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda akimkaribisha mgeni rasmi kuongea na wahitimu 

“Chuo chetu kwa idadi ya wanafunzi  asilimia 60 ni wenye jinsia ya kiume  na asilimia 40 ni wenye jinsia ya kike lakini inapokuja kwenye zawadi kwa waliofanya vizuri tunaona wasichana wanachukua asilimia 65 ya zawadi zote zilizotolewa kuliko wavulana na sisi kama menejimenti ya chuo tunadhani tatizo lipo kwenye nidhamu.

 “Wanafunzi wa kike wanaoneka kuwa wenye nidhamu wanaohudhuria madarasani bila kukosa wanafanya mazoezi yao waliyopewa na walimu wao na wanawasilisha kwa muda lakini kuna matatizo kwa baadhi ya wanafunzi wetu wa kiume ambao kwa kweli wengine hawaji madarasani  ama wanakuja lakini si inavyotakiwa ”, amesema Prof Chibunda.

Akizungumzia wanafunzi wenye jinsia ya kike kufanya vizuri chuoni hapo mmoja ya wahitimu SUA Halima Omary  amesema kuna muamko kubwa wa wasichana kushiriki katika tafiti na bunifu mbalimbali zinazoandaliwa chuoni lakini pia  uwepo wa sayansi na teknolojia umewasaidia sana kurahisisha katika usomaji wao hapo chuoni.



Post a Comment

0 Comments