Na Amina Hezron
Wananchi wameshauriwa kununua Miche ya miti ya matunda katika vyanzo vya uhakika pamoja na kufuata maagizo ya Wataalamu wa Kilimo wanayopewa kuhusiana na namna bora ya upandaji na utunzaji wa miche hiyo ya matunda ya muda mfupi pindi wanapoinunua ili kukidhi malengo waliyojiwekea.
Hayo yamezungumzwa na Meneja wa Kitengo cha Bustani katika Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Romani Mfinanga wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu miche hiyo ambapo kwa SUA chanzo chake ni Kitengo cha Bustani.
"Kumekuwepo na wajasiriamali wengine ambao wamekuwa wakitumia jina la Chuo kujitangaza kuwa na wao miche yao inatoka SUA kitu ambacho kiutaratibu si jambo jema hivyo wananchi wanapaswa kuchukua miche kwenye kitengo chetu ili wapate ushauri wa kitaalamu utakaowawezesha kufahamu namna ya kwenda kuikuza miche hiyo vizuri" alisema Mfinanga.
Akizungumzia kuhusiana na miche ya miembe ya muda mfupi amesisitiza kuwa njia nzuri ya kupata aina ya maembe uliyokusudia ni kuhakikisha machipukizi katika ncha shina yanaondolewa na mkasi au wembe mkali kwa kuwa yakiota yatasababisha upande wa kikonyo kushindwa kuendelea kukua.
"Kama yale machipukizi Mkulima atayasahau akayaacha yakaendelea kukua maana yake kile kikonyo na aina ya mche ambao ameukusudia kupata matunda ya aina fulani hatayapata tena kwasababu kile kikonyo kitafifia na kitakufa kwahiyo machipukizi yataendelea kukua na ndiyo yatakwenda kuwa mti wa matunda na mti huo hautoweza kuzaa ndani ya miaka mitatu kama inavyotakiwa, alisema Meneja huyo.
Amesema kitendo hicho cha kutokutoa machipukizi kitasababisha mti kuanza kuzaa baada ya miaka mitano na kuendelea hivyo ni muhimu kabisa mkulima akazingatia taratibu zote za namna bora ya uzalishaji wa miche ya matunda ili iweze kuzaa kwa wakati.
0 Comments