Na Amina Hezron
Katika kuhakikisha Wakulima wadogo wanaongeza uzalishaji na kuondokana na wimbi la umasikini, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Fair Planet umewakutanisha Wakulima zaidi ya 50 wanavyojishughulisha na Kilimo cha Mbogamboga kutoka kwenye Wilaya za Mvomero na Morogoro mkoani Morogoro kwa ajili ya kutambua aina bora za mbegu za mazao hayo pamoja na kujifunza mbinu bora za kilimo hicho zinazofanyiwa utafiti.
Mtafiti kutoka Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani (SUA) Dkt. Yasinta Zogela akizungumza na wakulima kuhusiana Malengo ya siku ya Mkulima Shambani katika Shamba la Mafunzo la SUA. |
Hayo yamebainishwa na Mtafiti kutoka Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani Dkt. Yasinta Zogela wakati akieleza malengo ya siku hiyo ya mkulima shambani iliyofanyika kwenye Shamba la Mafunzo la SUA ambamo majaribio hayo ya mbegu na teknolojia zake yanafanyika.
Amesema lengo ni kufanya tathmini ya mbegu mbalimbali za mazao ya bustani ambazo zinaweza kustahamili katika hali ya hewa ya uwanda wa juu yanayofanyika katika kata ya Mgeta na uwanda wa chini yanayofanyika SUA na baadae zikishafanyiwa tathmini na wakulima zikaonekana zinawafaa basi ziweze kutumika katika mashamba ya wakulima hao.
“Tuna Mbegu tofauti tofauti za mazao ya Bustani kutoka katika kampuni mbalimbali za Mbegu Duniani ambazo tumepitia hatua zote za kupata mbegu hizo ili tuweze kufanyia majaribio hivyo Wakulima watafahamu aina ya mbegu ambayo inastahamili Wadudu na magonjwa ikiwemo ugonjwa wa mnyauko ambao unasumbua sana hasa katika mazao ya bustani katika maeneo mbalimbali nchini”, alisema Dkt. Zogela.
Nae Mratibu wa Mradi huo Gal Nir kutoka Izrael amesema kuwa mradi huo umekuwa ukifanya majaribio hayo tangu mwaka 2019 ambapo wamekuwa wakichukua mbegu kutoka makampuni mbalimbali ya mbegu na kuzifanyia majaribio kuona uwezo wake kabla ya kuzipendekeza kwa wakulima kulingana na maeneo yao wanayolima lakini pia kuwapa nafasi kutembelea na kujifunza.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima wa mazao ya mbogamboga kutoka Kingolwira akiwemo Bw. Mayala Mabelele amewaomba Watafiti kutoka SUA kuwasaidia namna bora ya kuweza kukabiliana na changamoto ya Utitili katika kilimo cha vitunguu na ugonjwa wa Kanitangaze kwenye nyanya ili waepukane na matumizi ya viuatilifu ambavyo havionyeshi mafanikio.
Nae Afisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Zeno Assay amewataka wakulima hao waliopatiwa mafunzo kuhakikisha mafunzo waliyopata yanawafikia na wengine waliokosa nafasi hiyo ili na wao waweze kufahamu mbegu hizo zilizo kwenye majaribio na teknolojia bora za uzalishaji wa mazao ya mboga mboga. .
Mradi huo wa Fair Planet unafanya kazi zake nchini Ethiopia pamoja na Tanzania Mkoani Morogoro ambapo tayari umefanikiwa kutoa mafunzo kwa wakulima wa Hembeti, Mgeta, Kingolwir, Kipela na Mlali lakini mradi unatarajia kuendesha mafunzo katika maeneo mengine ya mkoa wa Morogoro na Nyanda za Juu Kusini.
Mkulima kutoka Kingolwira Manispaa ya Morgoro Bw. Mayala Mabelele akizungumza na SUAMEDIA jinsi alivyonufaika na Elimu iliyotolewa katika Siku ya Mkulima Shambani SUA. |
Mtafiti kutoka Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani (SUA) Dkt. Yasinta Zogela akifafanua jambo kuhusiana na Malengo ya Siku ya Mkulima Shambani pamoja na majaribio ya Mbegu na Teknolojia. |
0 Comments