Na: EDITHA MLOLI
Uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi umeonekana kupoteza fursa za ajira hapa nchini na badala yake kutengeneza ajira nje ya nchi na hii ni kutokana na uhaba wa sukari ambao ni kiasi cha tani elfu 60, huku mahitaji yakiwa ni tani laki 440 wakati Tanzania ikizalisha tani laki 380 pekee.
Kutokana na hali hiyo Serikali imeweka mikakati ya upanuzi, uboreshaji wa viwanda, pamoja na kuongeza uzalishaji wa sukari katika viwanda vikuu vinne vinavyozalisha sukari hapa nchini ambavyo ni Kilombero Sugar, TPC, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, ili kukabiliana na uhaba wa sukari na kupata akiba ya kuuza nje ya nchi.
Akizungumza Oktoba 25, 2022 na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuhusiana na Majukumu ya Bodi ya Sukari nchini kwa mwaka 2022/2023 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Prof. Keneth Bengesi amesema hadi kufikia mwaka 2025/2026 Serikali kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM inatarajia kuzalisha tani laki 7 kwa mwaka.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele kukaribisha wawekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo pia katika viwanda vya sukari ili kusaidia katika mkakati wa Serikali wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo katika maeneo yanayolima miwa ambapo viwanda hivyo vitasaidia kuzalisha sukari kwa wingi na kuongeza ushindani hapa nchini na kushuka kwa bei ya sukari nchini.
Prof. Bengesi amesema tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Sukari hapa nchini chini ya sheria Na. 26 ya mwaka 2001, bodi hiyo imekuwa na majukumu mengi ikiwemo kuzingatia ubora wa uzalishaji wa sukari lakini pia kuchangia asilimia 1% ya pato la Taifa, pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja na za muda.
Ameongeza kuwa kwa kuongeza viwanda vya uzalishaji wa sukari hapa nchini kwa kiasi kikubwa utaondoa uhaba wa sukari ambapo amesema kwa siku za hivi karibuni kumeongezeka baadhi ya viwanda kikiwemo cha Manyara Sugar ambacho kinazalisha tani elfu 8 kwa sasa, Bagamoyo Sugar kinachozalisha tani elfu 20, pamoja na Mkulazi kinachozalisha tani elfu 50.
0 Comments