Na Amina Hezron,Morogoro
Ili kupunguza idadi ya wanyama aina ya paka na mbwa wanaozurura mitaani Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya International Veterinary Outreach (IVO) kimetoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shahada ya Udaktari wa Wanyama SUA juu ya ustawi wa wanyama hao.
Kauli hiyo imetolewa na Mhadhiri Msaidizi wa Uzalishaji kutoka katika Ndaki ya Tiba za Wanyama na Afya ya Binadamu (SUA) Athanas Ngou wakati akitoa ufafanuzi juu ya mafunzo hayo yaliyoanza kufanyika oktoba 23 katika Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya ya Binadamu wakati akielezea lengo la mafunzo hayo.
Amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi hao wa namna ya kuwakinga wanyama dhidi ya magonjwa ikiwemo ugonjwa wa kichaa cha mbwa pamoja na magonjwa mengine ambayo yana madhara kwa binadamu pia ikiwemo ugonjwa wa mgunda ambao mbwa wanapatiwa chanjo.
“Hivyo katika kuwakinga hao mbwa na jamii pia itakuwa imekingwa kutokana kuwakinga mbwa hao lakini pia Chuo chetu tunahimiza sana wanafunzi wetu wapate mafunzo kwa vitendo, hii sasa ni nafasi kwa wanafunzi wetu kujifunza kwa vitendo namna ya kupunguza mbwa na paka”, alisema Ngou.
Nae Mwanzilishi wa International Veterinary Outreach (IVO) Dkt. Eric Eisenman amesema kuwa lengo lao ni kupunguza maumivu kwa wanyama na kuifanya jamii kuwa na afya hivyo walipata mawasiliano ya awali kutoka kwa taasisi zisizo za kiserikali mbili kutoka Tanzania ambazo zinazojishughulisha na ustawi wa wanyama.
“Tukaanza kuangalia namna gani tunaweza kushirikiana na kuwajengea uwezo watanzania ambao wanajishughulisha na uangalizi wa wanyama tukaona SUA ndio Chuo pekee kinachotoa elimu kwa watu juu ya masuala ya tiba za wanyama kwa kufundisha wanafunzi hivyo tukaona tufike SUA kuendesha mafunzo hayo”, alisema Dkt. Eisenman.
Amesema wametoa mafunzo kuhusiana na namna ya kumtunza na kumfanyia matibabu mbwa pamoja na kupunguza magonjwa yanayotoka kwa mbwa kwenda kwa binadamu ikiwepo kichaa cha mbwa lakini pia wamefundisha mbinu za msingi za namna ya kufanya upasuaji na kupunguza idadi ya mbwa.
Kwa upande wa wanafunzi waliopata nafasi ya kupata mafunzo hayo akiwemo Mwanafunzi wa Shahada ya Udaktari wa Mifugo (SUA) Haji Mkata amesema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kutambua haki ya wanyama pamoja na namna ya kuwamudu kwa kiwango walichopo mtaani kuwalinda na kuwafanya wasilete madhara katika jamii.
“Ningependa mafunzo haya yangekuwa endelevu ili kuongeza wanufaikaji wa mafunzo haya kwa kuwa ni mafunzo ambayo yanaonekana yana lengo kubwa la kutukomboa sisi katika fani zetu lakini kumkomboa mnyama na jamii pia”, alisema Mkata.
Mafunzo hayo ya siku tano yamefanyika siku mbili kwa nadharia huku siku zilizobaki yatamalizika kufanyika kwa vitendo katika kituo cha Tanzania Animal Welfare Society (TAWESO) kilichopo kibaingwa mkoani Dodoma.
0 Comments