Na Editha Mloli
Wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliochaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wameaswa kuwa na nidhamu, bidii, pamoja na kutojihusisha katika uhalifu wa aina yoyote utakaoweza kuharibu malengo yao pindi wawapo chuoni hapo, na badala yake kujitambua na kuzingatia kile kilichowaleta chuoni ili kutimiza ndoto zao.
Makamu Mkuu wa Chuo SUA Prof. Raphael Chibunda, akiwapongeza na kuwakaribisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na chuo. (Picha na Gojo Mohamed) |
Hayo yamezungumzwa Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof.
Raphael Chibunda, katika ukumbi wa Freedom Square, Kampasi ya
Solomon Mahlangu wakati akiwapongeza na kuwakaribisha wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na chuo hicho pamoja na kutoa maelekezo ya kuzingatia pindi wawapo
chuoni.
Prof. Chibunda amewataka wanafunzi hao kuzingatia
nidhamu na kuepuka makosa ya kimtandao yaani (Cyber Crimes), makosa ya
uzalilishaji wa kijinsia ambao mara nyingi unawalenga wanawake, lakini pia
amewataka kuwa mabalozi wazuri wa SUA, kuendana na teknolojia pamoja na kuwa na
matumizi mazuri ya muda.
Ameongeza kuwa wanafunzi wanapokuwa chuoni wapo huru na
hakuna anayewafuatilia hivyo kuwataka kuwa waangalifu sana na afya zao na
kujiepusha na magonjwa hasa UKIMWI na kuutumia muda vizuri wanapokuwa chuoni
ili kumaliza kwa wakati waliopangiwa na kufikia ndoto zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shahada za Awali wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Nyambilila Amuri amewataka wanafunzi
kukamilisha usajili kwa muda wa siku 14 waliopangiwa hadi Novemba 16, 2022, ili
kuepuka usumbufu utakaojitokeza.
Dkt. Nyambilila pia amewataka wanafunzi kutokuiba kazi
za watu wengine na kudai kuwa ni kazi zao, lakini pia kutokufanya udanganyifu
katika kipindi cha mitihani kwani ukikamatwa unafanya udanganyifu unaweza
kufukuzwa chuo hivyo kuwataka kuwa waangalifu juu ya hilo.
Wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga na SUA wakifuatilia kwa umakini maelekezo katika Siku
ya Utambulisho wa Chuo uliofanyika katika Kampasi ya Solmon Mahlangu. (Picha na Gojo Mohamed) |
0 Comments